Watibu mishipa ya moyo kwa kutumia ya mikononi

KWA mara ya kwanza nchini, Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), ikisaidiana na madaktari bingwa watatu kutoka nchini Saudi Arabia, wametoa utaalamu mpya wa kutibu mishipa ya damu ya moyo iliyoziba kwa kutumia mishipa ya mikononi.

Kabla ya teknolojia hiyo mpya, walitumia tiba kwa kutumia mishipa ya paja ambayo ilimlazimu mgonjwa baada ya matibabu kukaa hospitalini kwa siku nne, lakini kwa njia hii mpya mgonjwa anapumzika kwa saa nne tu kisha anaruhusiwa kwenda nyumbani.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo na Mkurugenzi wa Tiba ya Moyo (JKCI), Peter Kisenge alisema jana alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. Dk Kisenge alisema teknolojia hiyo mpya imeokoa gharama ya zaidi ya Sh milioni 800 ya wagonjwa 40 ambao wanatarajiwa kutibiwa kwa siku nne katika kambi hiyo ya siku nne iliyowekwa hospitalini hapo tokea juzi hadi kesho.

Pia imepunguza idadi ya wagonjwa waliokuwa wanakwenda kutibiwa nje ya nchi kutokana na matatizo hayo ya kutibu wagonjwa wa mishipa ya damu ya moyo. “Utaalamu huu mpya unapunguza gharama za hospitalini pamoja na za serikali za kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi.

Mpaka leo mchana (jana) tayari wagonjwa 13 wameshafanyiwa tiba hiyo tunatarajiwa tufikapo mwisho wagonjwa 40 watakuwa wametibiwa,” alieleza Dk Kisenge. Alisema madaktari hao kutoka Saudi Arabia, pia wapo kwa ajili ya kuifundisha teknolojia hiyo mpya kwa madaktari wa taasisi hiyo.

Kwa upande wake, Dk Ali Almasood kutoka Saudi Arabia alishukuru kwa kufanikisha tiba kwa wagonjwa ambao tayari wamewatibu, kwani wanaendelea vizuri pia alisema wapo kwa ajili ya kutoa utaalamu huo kwa madaktari wa JKCI.

Mgonjwa Elly Palangyo ambaye amefanyiwa tiba hiyo, aliwashukuru madaktari hao na kuwataka Watanzania waache mawazo ya kwenda kutibiwa nje ya nchi kwa kuwa huduma nzuri zinapatikana katika taasisi hiyo ya moyo.