Wagonjwa watumika kusafirisha ‘unga’

WABUNGE wametaja njia zinazotumika kuingizwa dawa za kulevya nchini na kusafi rishwa nje ya nchi, ikiwemo wagonjwa kubebeshwa dawa hizo na kupita katika viwanja vya ndege.

Sambamba na hilo, imeelezwa kuwa dawa hizo pia huingizwa nchini kupitia viwanja vya ndege ‘bubu’ , bandari bubu na uwanja wa ndege sehemu ya watu mashuhuri.

Wabunge walibainisha njia hizo jana wakati wakichangia Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya wa mwaka 2017 ambao uliwasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama.

Marekebisho ya muswada huo yalipitishwa. Mbunge wa Tanga Mjini, Mussa Mbarouk (CUF) alisema sasa hivi wagonjwa wanabebwa kwenye baiskeli maalumu za wagonjwa huku wakisindikizwa na ndugu zao wenye mizigo na wanapofika sehemu ya kukaguliwa wanaelezwa lifti imeharibika na kupitishwa eneo lisilokuwa na ukaguzi.

Alisema mgonjwa huyo na waliomsindikiza wanakuwa wamebebeshwa dawa za kulevya na kuingiza nchini ama kusafirishwa nje. Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Lulida (CUF) alisema Tanzania ina viwanja vya ndege 58 na kati ya hivyo tisa pekee ndivyo vilivyo na maofisa wa serikali huku vilivyobaki vipo kwenye mbuga na maeneo mengine ya siri kama ukanda wa pwani ambapo hutumika kuingiza dawa za kulevya nchini.

“Wanaoingiza dawa za kulevya wanapitishwa kule VIP (sehemu ya watu mashuhuri), pale uwanja wa ndege Dar es Salaam (JNIA) watu wachovu tu wanapita pale bila kukaguliwa lakini sisi kwenye nchi za nje hatuthaminiwi hata kupita VIP zao, bandari bubu zinaingiza dawa za kulevya na ukanda wa Pwani ndiyo umeathirika zaidi,” alisema.

Kwa upande wake Mbunge wa Mjimkongwe, Ally Saleh (CUF) aliitaka serikali kufuatilia uuzaji wa dawa za kulevya kupitia mitandao ya kijamii kwani kwa sasa mitandao hiyo inatumika kwenye biashara ya kuuza ngono ambapo mtu anaelekezwa wapi atapata huduma hizo.

Alitaka sheria isiangalie kuadhibu zaidi wanaotumia dawa za kulevya kwani wanapokuwa gerezani wanapata maradhi kama virusi vya Ukimwi hivyo akashauri ni vema kutiwa mkazo kuwapatia elimu watumiaji wa dawa hizo.

Naye Mbunge wa Muheza, Adadi Rajabu (CCM) alisema makosa ya kukutwa na bangi na mirungi kilo 50 na adhabu yake ya kifungo cha maisha ni adhabu kubwa kwani kiwango hicho ni kidogo, hivyo kitasababisha watu wengi kufungwa na kuleta msongamano magerezani.

Akijibu hoja za wabunge; Waziri Mhagama alisema ameiagiza Mamlaka za Kupambana na Dawa za Kulevya za Zanzibar na Tanzania Bara kukutana kupanga mikakati ya kupambana na vita hiyo ya dawa hizo.

“Adhabu ikiwa kubwa ndiyo vizuri itafanya biashara iwe ghali na hiyo itasaidia kuokoa Watanzania wengi na tunaamini sheria hii itapunguza matumizi na biashara hii,” alisema. Alisema serikali itafungua vituo vya tiba ya methadone kwa watumiaji wa dawa za kulevya katika mikoa ya Dodoma, Mbeya na Mwanza.

Kwa sasa kuna vituo vitatu na vyote vipo mkoani Dar es Salaam. Alisema serikali inanunua kilo moja ya methadone kati ya dola za Marekani 650 na 1,500 na sasa imeanza kununua nchini India. “Mwaka 2016 tulinunua kilo 120 za methadone kwa dola za Marekani 180,000 na mwaka huu tumenunua kilo 300 kwa dola za Marekani 450,000,” alisema