Kinyerezi II yaandaliwa kuingizwa kwenye gridi

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limeanza maandalizi ya kukiunganisha Kituo cha Uzalishaji Umeme wa Gesi cha Kinyerezi II kilichopo jijini Dar es Salaam katika Gridi ya Taifa ili kuongeza kiwango cha umeme nchini.

Aidha kazi hiyo inakwenda sambamba na kazi ya usafishaji na uungaji wa bomba kubwa la gesi katika mitambo ya uzalishaji umeme ya Kinyerezi I, hatua ambayo pia inalenga kuongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme nchini.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Meneja wa Uhusiano wa Tanesco, Leila Muhaji alipokuwa anazungumzia mpango huo wa Tanesco. Alisema kukamilika kwa uunganishaji wa Kituo cha Umeme wa gesi cha Kinyerezi II katika Gridi ya Taifa kutaongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme kwa kuongeza megawati 30 ifikapo Desemba mwaka huu.

Kutokana na kazi hizo kubwa zilizoanza kufanywa na shirika hilo jana na kutegemewa kumalizika leo, Tanesco imetangaza kutokea kwa upungufu wa umeme katika maeneo mbalimbali nchini.

Pia shirika hilo limetoa taarifa kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini kuifahamisha kuzuia ndege kuruka katika anga la eneo la Kinyerezi kutokana na hatari inayoweza kusababishwa na kazi hiyo.

Muhaji alisema kutokana na kazi hiyo wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wameonywa kutopita karibu na eneo la mitambo hiyo ya kuzalisha umeme ya Kinyerezi hadi pale kazi hiyo itakapokamilika.

“Kutokana na kazi hii wananchi mnaombwa msipite karibu na eneo la mitambo ya Kinyerezi, kutokuwasha moto, kutokufanya shughuli za uchomeleaji vyuma pamoja na shughuli yoyote yenye viashiria vya moto ili kujikinga na madhara yanayoweza kutokea,” alisema Muhaji.