Waziri Mkuu aomboleza kiongozi CWT

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameungana na wanafamilia, viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) katika kuomboleza kifo cha Katibu Mkuu wa CWT, Yahya Msulwa nyumbani kwake, Tuangoma jijini Dar es Salaam.

Msulwa amefariki dunia juzi katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu. Waziri Mkuu aliambatana na mkewe Mama Mary Majaliwa. Akizungumza kwa niaba ya serikali, Waziri Mkuu alisema kifo hicho ni pigo kwa serikali kwa sababu marehemu alishirikiana nayo vizuri akiwa kiongozi wa walimu ambao ni zaidi ya asilimia 65 ya watumishi wa umma.

Waziri Mkuu alisema kuwa marehemu alikuwa mchapakazi na mwenye ushirikiano mzuri na wenzake na kuwa Novemba 12, 2017 alipokea barua kutoka CWT iliyosainiwa na marehemu akimualika kushiriki kwenye shughuli za chama.

“Wote tumeguswa na msiba huu, marehemu alikuwa mtumishi wa muda mrefu wa Chama cha Walimu Tanzania tangu mwaka 1996 na alikuwa rafiki na ndugu wa kila mmoja. Alikuwa na tabia njema, hivyo tunatakiwa kuyaenzi mambo mema aliyotuachia,” alisema.

Waziri Mkuu aliongeza kuwa ni wajibu wa watu wote kumuombea kwa Mwenyezi Mungu, ili ailaze roho yake mahali pema na kuwaomba wanafamilia, mke wa marehemu na watoto kuwa na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao.