Panzi mwenye bendera ya taifa kuibeba Moro

WANANCHI zaidi ya 151,000 wanaoishi katika vijiji 62 vinavyozunguka Hifadhi ya Mazingira Asili Uluguru (UNFR), mkoani Morogoro wanatarajia kunufaika kiuchumi na mapato yatokanayo na Utalii wa vivutio adimu vilivyomo katika hifadhi hiyo akiwemo panzi mwenye rangi ya bendera ya taifa la Tanzania.

Kaimu Mhifadhi wa Hifadhi hiyo, Mohamed Borry alisema hayo juzi kwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali waliotembelea Ofisi ya Hifadhi hiyo walipokuwa katika mafunzo ya siku tano ya Uandishi wa habari za Mazingira.

Mafunzo hayo yamegharamiwa na serikali ya Sweden kupitia Shirika lake la Kimataifa la Maendeleo (SIDA) na kuratibiwa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa habari za mikoa Tanzania (UTPC).

Alisema kwa sasa wameanza kuboresha miundombinu katika kambi ya kupokea watalii iliyopo eneo la Bunduki ili iweze kupokea idadi kubwa ya watalii na baadaye kuboresha maeneo mengine ya vivituo vya utalii ikiwemo Lukwangule, Bondwa, Hululu, Kinole, Tegetero, Moring Side na Lupanga.

Borry ambaye ni Ofisa Misitu alisema moja ya eneo lililowekewa kipaumbele ni kumtangaza panzi huyo mwenye rangi ya bendera ya taifa na mwingine mwenye alama ya namba tisa mgongoni. “Panzi hawa ni kivutio kitakachoingiza mapato ya utalii katika hifadhi hii na wananchi kunufaika na sehemu ya mapato haya,” alisema Borry.

Hata hivyo, alisema panzi wenye alama ya namba tisa mgogoni hupatikana eneo la safu ya Milima la Uluguru na hupendelea kuonekana siku ya Desemba 9 ambayo ni siku ya Uhuru.

“Panzi huyu mara ya mwisho imelezwa alionekana miaka 20 iliyopita, lakini kwa mara ya kwanza tangu kipindi hicho ameonekana tena mwanzoni mwa Novemba mwaka huu na hii inaonesha kuwa wananchi wameanza kutunza mazingira na kusababisha uoto wa asili kuimarika,” alisema.

Borry alivitaja vivutio vingine ni pamoja na aina tatu ya jamii ya vyura ambao hawapatikani sehemu nyingine isipo kuwa katika hifadhi hiyo ni mwenye mguu moja, miwili na mitatu, wakiwemo pia vinyonga wenye pembe moja, mbili na tatu.

Naye Ofisa misitu katika hifadhi hiyo, Lorubare Simon alisema Hifadhi inashirikiana na jamii katika utunzaji wa mazingira ikiwa na ugawaji wa mizinga ya nyuki na mafunzo ya shughuli mbadala kama ufugaji wa samaki na bustani za mboga.