Yanga kufa na Mbeya City

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga watakuwa wenyeji wa Mbeya City leo katika mchezo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru.

Yanga yenye pointi 17 itahitaji ushindi kujihakikishia nafasi yao ya utetezi wa taji hasa baada ya mchezo uliopita kushindwa kufanya vizuri ugenini dhidi ya Singida United kwa kulazimishwa suluhu.

Mbeya City siyo timu ndogo pia, wala hawafai kubezwa wanaweza kubadilisha matokeo, ingawa Yanga inapewa nafasi kutokana na faida ya uwanja wa nyumbani. Msimu uliopita Yanga ilishinda 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa ingawa walikuja kufungwa na Mbeya City 2-1 kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya katika mechi ya marudiano.

Kila mmoja ameshacheza michezo tisa. Timu hiyo ya Mbeya ina pointi 11 ambazo haziwatoshi kuridhika, hivyo ni lazima wapambane kupata matokeo mazuri. Ikiwa watafungwa huenda wakashuka katika nafasi waliopo na wengine kupanda juu.

Timu zote mbili zina wachezaji waliotoka pande mbili ambapo Yanga ina Raphael Daudi aliyesajiliwa msimu huu kutoka Mbeya City, hivyo utakuwa ni mchezo wake wa kwanza dhidi ya timu yake ya zamani.

Pia, mkongwe Mrisho Ngasa aliyeko Mbeya City aliwahi kukipiga Yanga lakini msimu uliopita hakuifunga timu yake hiyo ya zamani walipokutana. Yanga bado ina wachezaji wengi majeruhi akiwemo Donald Ngoma, Thaban Kamusoko, Papy Tshishimbi huku Amis Tambwe akitarajiwa kurudi taratibu baada ya kuanza mazoezi.

Ushindi hasa kwa Yanga utakuwa na faida kwao kupigania tatu bora kwa sababu ushindani wa namba umekuwa mkali kutoka timu za Azam, Mtibwa na Simba. Azam FC itakuwa ugenini dhidi ya Njombe kwenye Uwanja wa Sabasaba.

Ni mchezo mgumu kwa Njombe Mji ambao wanashika nafasi ya tatu kutoka mwisho wakiwa na pointi saba katika michezo tisa. Timu hizo ziliwahi kukutana katika mechi ya kirafiki kwenye maandalizi ya ligi ambapo Njombe ilishinda 2-0. Lakini leo ni mchezo wa mashindano lolote linaweza kutokea pengine kwa Azam au Njombe.