Serikali: Tunazingatia sheria kudhibiti mifugo kutoka nje

SERIKALI imesema hatua inazochukua dhidi ya mifugo inayoingia nchini kinyume cha sheria zimezingatia taratibu, sheria za nchi, makubaliano ya kikanda na kimataifa.

Katika taarifa iliyotolewa jana, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa vyombo vya habari ilibainisha kuwa, hatua zote zilizochukuliwa na serikali dhidi ya mifugo iliyokamatwa, zilifanyika kwa mujibu wa sheria na makubaliano hayo. Ilisema kumekuwepo taarifa katika baadhi ya vyombo vya habari na baadhi ya wanasiasa zinazoishutumu serikali kutokana na hatua ya kukamata na kupigamnada mifugo iliyoingizwa nchini bila kufuata sheria.

Aidha, taarifa hiyo ilisema taarifa hizo zinajenga sintofahamu kuhusu suala la vifaranga vya kuku vilivyoteketezwa baada ya kuingizwa nchini bila kufuata sheria. Ilisema kabla serikali haijachukua hatua yoyote dhidi ya mifugo iliyoingia nchini wakiwemo vifaranga hao, huwasiliana na serikali za nchi husika kupata ufafanuzi.

“Kuhusu suala la vifaranga, serikali ya Kenya ilimwita Balozi wetu aliyeko Nairobi kutaka maelezo. Balozi wetu alisikiliza maelezo ya serikali ya Kenya na akatumia fursa hiyo kuelezea masuala haya kwa serikali ya Kenya.

Vile vile serikali imepokea barua kutoka serikali ya Kenya kuhusu masuala haya, na serikali itaijibu barua hiyo kutoa ufafanuzi,” ilisema taarifa hiyo iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika wizara hiyo.

Ilitaja baadhi ya sheria hizo kuwa ni Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Namba 17 ya Mwaka 2003 na Kanuni zake za mwaka 2007 na 2010, zinazotumika kudhibiti na kukagua uingizaji wa mifugo na mazao yake katika maeneo ya mpakani, bandarini na viwanja vya ndege.

Pia Sheria ya Nyanda za Malisho na Rasilimali ya Vyakula vya Wanyama Namba 13 ya mwaka 2010 inayosimamia nyanda za malisho na ubora wa malighafi za kusindika vyakula vya mifugo na zuio la uingizaji ndege na mazao yake nchini la mwaka 2006, kutokana na uwepo wa ugonjwa hatari wa homa ya mafua makali ya ndege katika nchi mbalimbali duniani.