Museveni, Kagame wataka soko la pamoja Afrika

RAIS Yoweri Museveni wa Uganda na Rais wa Rwanda, Paul Kagame wanataka nchi za Afrika, ziungane katika kuzitumia fursa za kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kuwa na soko la pamoja kwa faida ya nchi hizo na bara zima kwa ujumla. Kwa nyakati tofauti, marais hao walitoa kauli zenye mwelekeo huo.

Kuanzia Novemba 13 hadi 17 Baraza la Kisekta la Jumuiya ya Afrika Mashariki la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) lilikutana jijini Arusha, kujadili masuala kadhaa ukiwemo utekelezaji wa mapendekezo ya kuwa na soko la pamoja. Majadiliano yanaendelea kuanzisha Soko la Pamoja Afrika (FTA) na yamepangwa kukamilika Desemba mwaka huu. Majadiliano hayo yalianza Juni mwaka 2015.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Biashara, Forodha na Masuala ya Fedha wa Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA), Dk Francis Mangeni alitahadharisha kuharakisha kukamilisha jambo hilo, kwakuwa nchi zinaweza kupata matatizo ya kujitakia. Wakati wa Mkutano wa Nne wa Dunia wa Biashara Kuhusu Africa (AGBF) uliofanyika hivi karibuni kwenye Falme za Nchi za Kiarabu (UAE) jijini Dubai, Rais Museveni alisema anatamani atakapoondoka madarakani, aiche Afrika ikiwa na soko la pamoja.

“Ningependa kuona soko moja la pamoja kwa ajili ya Afrika. Pia ningependa kuona jumuiya kubwa zaidi za kisiasa tujilinde kwenye dunia ya mataifa makubwa,” alisema Rais Museveni. Katika mkutano huo, Museveni pia alisema, anataka kuiacha Afrika yenye vichocheo vikubwa vya uzalishaji.

“Watu hawaelewi kwamba nchi 54 Afrika haziwezi kufanikiwa kama haziungani hasa kiuchumi na kisiasa,” alisema kwenye mkutano huo, uliojadili namna ya kuongeza uwekezaji barani Afrika. Kwa mujibu wa Rais Museveni, ili kizazi kijacho kimudu changamoto zilizopo, jambo la msingi si tu kuwa na umoja wa kisiasa ila pia soko la pamoja.

Alisema, Afrika tayari ni eneo linalofaa kwa ushirikiano wa uwekezaji na mataifa mengine duniani. Alitaja baadhi ya vivutio muhimu Afrika kuwa ni uwepo wa maliasili, soko linalokua, amani kwenye nchi nyingi, jumuiya mbalimbali ikiwemo ya Afrika Mashariki, miundombinu bora ikiwemo ya mtandao wa usafirishaji na umeme. Katika mkutano huo wa AGBF, Rais Kagame alisema kilichofanyika kuanzisha jumuiya za kiuchumi Afrika kifanyike kupata rasilimali ili bara hilo liwe eneo moja lenye tija.

Alisema jambo hilo ni muhimu. Alitoa mfano kwamba EAC kwamba, imekuwa na mafanikio chanya ukiwemo uhuru wa watu kwenda popote, umoja wa forodha na miradi ya pamoja ya miundombinu.

Mkutano huo ulioandaliwa na Taasisi ya Viwanda na Biashara ya Dubai, ulihudhuriwa na viongozi wakuu wa serikali, wafanya uamuzi kwenye mashirika na taasisi na wataalamu wa viwanda ukiwa na kaulimbiu ‘Kizazi Kijacho Afrika”. Wajumbe kwenye mkutano huo, walitathmini hali ya sasa ya uchumi barani Afrika na matarajio yake kwenye maendeleo, fursa za uwekezaji zikiwemo za ushirikiano wa biashara za barani humo na wenzao wa UAE.

Rais Kagame alieleza umuhimu wa Afrika kuwa na ajenda ya mfuko utakaozidisha mtangamano barani humo sanjari na kuongeza matarajio kidunia. Kwa mujibu wa Kagame, mtangamano na ushirikiano wa karibu baina ya jamii za nchi wanachama, utaharakisha maendeleo na ustawi wa nchi husika. Alisema, mtangamano wa kieneo barani Afrika utawezesha kuondoa migawanyiko ambayo kwa muda mrefu umekuwa kikwazo kwa ustawi wa bara hilo.

“Kama ukitazama eneo la Afrika Mashariki, maendeleo makubwa yamepatikana, kwa mfano, kwenye eneo la umoja wa forodha, mtangamano kwenye eneo la miundombinu inayoziunganisha pamoja nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, iwe kwenye mawasiliano ya simu likapatikana eneo moja na mtandao (OAN) na hakuna gharama za kupiga simu kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine (roaming charges),” alisema Rais Kagame.

Mwaka 2014 nchi nne wanachama EAC ikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda na Sudan Kusini zilikubaliana kuwa na eneo la pamoja la mtandao wa simu, hivyo kupunguza gharama za mawasiliano. “Historia ililigawa bara na hili lilizuia Afrika kufanikiwa kama ambavyo ingekuwa. Leo Waafrika wanafanya kazi pamoja zaidi kwenye ulinzi, uchumi na siasa pamoja na historia ya mgawanyiko ambayo ililigawa bara