Noni, wenzake kortini kwa uhujumu uchumi

VIGOGO wanne wa Kampuni ya Six Telecoms Limited akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi wa Rasilimali watu benki ya TIB, Peter Noni wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi, ikiwemo kusababisha hasara ya Dola za Marekani milioni 3.7 sawa na bilioni nane na utakatishaji fedha.

Mbali na Noni ambaye pia ni Mfanyabiashara na Mkurugenzi wa kampuni hiyo, wengine ni Mhandisi na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Hafidhi Shamte, Mhadhiri na Mkurugenzi wa kampuni hiyo Ringo Tenga, Mkuu wa fedha wa kampuni hiyo, Noel Chacha na Kampuni ya Six Telecoms Limited.

Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo majira ya saa 3 asubuhi na kusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali, Jehovaness Zacharia mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa.

Zacharia alidai katika kesi hiyo namba 73 ya 2017, kuwa kati ya Januari Mosi 2014 na Januari 14, 2016 maeneo ya jiji la Dar es Salaam, washitakiwa wote kwa pamoja, walitoza malipo ya mawasiliano ya simu za kimataifa chini ya kiwango cha dola 0.25 kwa dakika kwa lengo la kujipatia faida binafsi.

Alidai kuwa katika siku hizo hizo washitakiwa kwa udanganyifu na kwa nia ya kuepuka malipo, walishindwa kulipa kiasi cha dola za Marekani 3,282,741.12 kama mapato kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). Pia alidai kuwa washitakiwa hao wanadaiwa kushindwa kulipa ada za udhibiti wa mawasiliano ambazo ni dola za Marekani 466,010.07 kwa TCRA.

Katika mashitaka ya utakatishaji washitakiwa Shamte, Noni,Tenga na Chacha wanadaiwa kujipatia, kutumia na kusimamia dola za Marekani 3,282,741.12 wakati wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya udanganyifu yanayotokana makosa mengine wanayoshitakiwa nayo.

Zacharia alidai katika mashitaka ya tano kuwa Kampuni ya Six Telecoms ilijipatia, ilitumia na kusimamia dola za Marekani 3,282,741.12 wakati ikijua fedha hizo ni zao la makosa ya udanganyifu. Inadaiwa washitakiwa wote kwa pamoja waliisababishia TCRA hasara ya dola za Marekani 3,748,751.22 ambayo ni sawa na Sh bilioni nane.

Washitakiwa hao hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi zinazozidi gharama ya Sh milioni 10 hata hivyo, upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika. Wakili wa utetezi, Dk Masumbuko Lamwai aliiomba mahakama kukataa mashitaka dhidi ya washitakiwa na kuomba iwaambie upande wa mashitaka wakaandae upya mashitaka yao na kuwaleta mahakamani.

Dk Lamwai alidai mashitaka dhidi ya washitakiwa hao yameletwa haraka haraka na kwamba mashitaka hayako sawa. ‘’Mashitaka haya hayaoneshi mshitakiwa yupi katenda kosa gani, pia hati ya mashitaka ilitakiwa kuonyesha makosa,’’ alidai Lamwai. Hata hivyo, Hakimu Nongwa aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 24 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Washtakiwa walirudishwa rumande kwa kuwa mashitaka ya utakatishaji fedha hayana dhamana.