Utendaji wa Magufuli waibomoa Chadema

WANASIASA sita kutoka vyama vya upinzani wamejiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kupokewa rasmi na Halmashauri Kuu ya chama kilichoketi Ikulu jijini Dar es Salaam jana chini ya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli.

Aidha, sababu za kisera, kiitikadi na ya kiutawala chini ya Rais Magufuli ndiyo yanayotajwa na wanasiasa hao kuwa sababu ya kuvihama vyama walivyokuwa wanachama. Waliojiunga na CCM jana ni pamoja na aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha ambaye alihamia Chadema baada ya Uchaguzi Mkuu Zaidi ya 3,000 wawania uongozi CCM uliopita na Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana Chadema (BAVICHA), Patrobas Katambi.

Wengine waliojiunga na chama hicho ni waliokuwa wanachama cha ACT-Wazalendo akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo ambaye aliwahi kuwa kiongozi wa chama hicho, Samson Mwigamba, Edna Sungu na Wakili wa kujitegemea wa chama hicho, Albert Msando.

Pia aliyewahi kuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba ambaye naye amerejeshwa CCM baada ya awali kuvuliwa uanachama kwa madai ya kukisaliti chama kwenye uchaguzi huo mkuu wa mwaka 2015. Akizungumza kwenye mkutano huo, Rais Magufuli aliwaonya wanasiasa hao waliorudi CCM kutofanya hivyo kwa majaribio, bali wamaanishe na wakitumikie chama kwa uaminifu.

Alisema kuwa CCM imekuwa imeendelea kufanya mageuzi makubwa tangu mwaka jana kwa nia ya kukirejesha chama kwenye misingi yake, ikiwemo kukirudisha kwa wanachama ili kiwatumikie wananchi pamoja na kuondoa taswira hasi dhidi ya chama, ikiwemo kuporomoka kwa maadili. Akiomba kurudi CCM, Masha alisema: “Naomba mnikubali kwa kuwa mimi ni mwana mpotevu.

Na kwa kuwa mnasema ng’ombe aliyekatwa mkia huwa anaangaliwa mara mbilimbili, mimi naomba niwaambie sijakatwa mkia na niko imara”. Kwa upande wake, Profesa Mkumbo alisema ameamua kurudi CCM kutokana na kasi kubwa ya mageuzi yanayofanyika ya kukifanya watu wakitumikie Chama na siyo Chama kuwatumikia watu. Alisema kumekuwa na mageuzi makubwa kisera, kiitikadi na maeneo mbalimbali ya kiutawala na hivyo kuwafanya watu kukiogopa CCM na siyo CCM kuogopa watu.

Naye Edna alisema: “Naomba kujiunga na CCM kwa sababa CCM mnapambana na rushwa na ufisadi kivitendo. CCM ina dhamira ya dhati kuirudishaTanzania kwenye misingi kwa kupambana na wizi, dhuluma na unyonyaji wa rasilimali za nchi”.

Naye aliyekuwa Mwenyekiti wa Bavicha, Katambi alisema ameachana na kundi la wabinafsi, hivyo ameamua ajiunge CCM kwa ajili kutetea maslahi ya taifa. Aliongeza kwamba kuna watu wanapenda mabadiliko lakini wenyewe hawataki kubadilika na yanapotakiwa kuja mabadiliko hutokea misuguano mingi. Alisema wanasiasa wengine wanatenda na kuishi tofauti na wanachosema.

Akizungumzia kujiunga na CCM, Mwigamba alisema kuwa ameamua kujiunga na CCM kwa kuwa ni chama kinachotekeleza Ilani yake kwa vitendo ikiwemo kutoa huduma bora za jamii kama afya kwa kuhakikisha dawa zinapatikana, kusimamia rasilimali za nchi kwa kufanya mabadiliko ya sheria kadhaa ikiwemo ya madini, majadiliano na wawekezaji, hivyo kuondoka kwake kwenda CCM ni kutaka kuwa moto na kukataa uvuguvugu.

Naye Msando alisema: “Sikuwahi kuwa mwana CCM, ni mara ya yangu ya kwanza kujiunga na chama hiki, nimefanya hivyo kwa sababu naiona CCM mpya, zamani ilikuwa shida kwa mtu kujitambulisha kama mwana CCM”.

Kuhusu msamaha wa Sophia Simba, Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa nchi, Dk Magufuli alisema ameandika barua kadhaa ikiwemo ya Machi 14 mwaka huu akiomba msamaha na kujutia makosa aliyoyafanya hadi akavuliwa uanachama wa CCM Magufuli aliwahoji wajumbe wa NEC ambao wote kwa kauli moja walikubali asamehewe.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Bashiru Ally alisema kuwa hakuna tatizo kwa wanasiasa kuhama kutoka chama kimoja kwenda kingine kwa kuwa wanatumia hiari, uhuru na haki yao ya kisiasa. Hata hivyo, Dk Bashiru alisema kuwa ni vigumu kujenga nchi yenye umoja na kupiga hatua za kimaendeleo kama hakuna vyama vya siasa madhubuti.

Alisema makundi kwa misingi ya ukabila, udini na ukanda ambayo yameanza kujionesha hayasaidii katika kujenga taifa. “Wanasiasa wanatakiwa kujenga vyama madhubuti ili kusaidia kujenga nchi yenye maendeleo,”alisema.