Utafiti Twaweza: Rushwa imepungua

MATOKEO ya utafi ti wa Twaweza yameonesha kuwa asilimia 85 ya wananchi wanaripoti kuwa, viwango vya rushwa vimepungua nchini kwa mwaka 2017 ikilinganishwa na mwaka 2014 ambao asilimia 78 walisema viwango vya rushwa vilikuwa vikubwa kuliko miaka 10 iliyopita.

Aidha, utafiti huo umebainisha kwamba, wananchi wameripoti kuwa uzoefu wao wa kuombwa rushwa umepungua katika sekta zote mwaka huu ikilinganishwa na 2014. Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze alisema matokeo hayo yametolewa kupitia utafiti uitwao: “Hawashikiki?

Mitazamo na maoni ya Watanzania juu ya Rushwa.” “Utafiti huu unatokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mkononi.

Matokeo hayo yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,705 kutoka maeneo mbalimbali Tanzania Bara kati ya Julai na Agosti mwaka huu,” alibainisha Eyakuze.

Alisema matokeo hayo ya utafiti yanatia matumaini ikilinganishwa na miaka mitatu iliyopita, ambako wananchi wamekuwa na mtazamo chanya kuhusu mafanikio yanayojitokeza kutoka katika mapambano dhidi ya rushwa.

Mwakilishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Sabina Seja alisema rushwa bado ipo na kuwataka wananchi na wadau mbalimbali kutoa ushirikiano katika kupambana nayo badala ya kuiachia serikali pekee.

Naye Ludovick Utouh aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), alisema ni kweli kwa kipindi hiki rushwa imepungua tofauti na miaka ya nyuma na kuwataka Watanzania kuichukia rushwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, alisema wananchi wanaripoti kuombwa rushwa katika sekta mbalimbali kumepungua ambapo kwa upande wa polisi ilikuwa asilimia 60 mwaka 2014 hadi asilimia 39 mwaka 2017, Ardhi asilimia 32 mwaka 2014 hadi asilimia 18 mwaka huu, Afya asilimia 19 mwaka 2014 hadi asilimia 11 mwaka huu.

Kuhusu sekta ya maji, wananchi waliripoti kuombwa rushwa kwa asilimia 20 mwaka 2014 na kwa mwaka huu ni asilia sita, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) asilimia 25 mwaka 2014 na asilimia tano mwaka 2017, na Asasi zisizo za kiserikali (NGOs) ni asilimia 13 na asilimia sita kwa mwaka huku.

“Sekta pekee ambayo rushwa iliripotiwa kubaki vilevile ni sekta ya ajira ambapo asilimia 34 ya wananchi waliripoti kuombwa rushwa mwaka 2014, huku asilimia 36 wakiombwa rushwa mwaka 2017,” alieleza mtendaji huyo wa Twaweza.

Alisema pengine kutokana na uzoefu wa viwango vikubwa vya rushwa, wananchi wengi wamepata matumaini juu ya mapambano dhidi ya rushwa, mwaka 2014 zaidi ya nusu ya wananchi ambao ni asilimia 51 walisema rushwa haiwezi kupungua nchini, wakati mwaka 2017 asilimia 63 ya wananchi wanasema itaweza kupunguzwa kwa kiwango fulani.

Alisema pamoja na mtazamo wa wananchi kwamba rushwa imepungua, sekta za polisi na mahakama bado zinaongoza kwa rushwa, kwani asilimia 39 na asilimia 36 ya wananchi wanasema waliombwa rushwa mara ya mwisho walipokutana na taasisi hizo mbili.

“Maelezo ya wananchi ya maana ya rushwa ni utoaji wa fedha wakati wa kampeni asilimia 93, utoaji wa fedha na vitu kwa ajili ya kupata huduma asilimia 78 na kuwalipa wafanyakazi hewa asilimia 65.

Asilimia 51 wanasema posho za vikao ni rushwa, lakini ni asilimia tatu tu wanaosema wafanyabiashara kutoa fedha kusaidia kampeni za uchaguzi na kisha kutarajia msaada ni rushwa,” aliongeza Eyakuze kuhusu matokeo ya utafiti huo.

Aidha, alisema wananchi wengi wanataka wanaopatikana na hatia ya rushwa wafungwe gerezani na adhabu hiyo ilichaguliwa zaidi kwa askari wa barabarani aliyechukua rushwa ya Sh 20,000 asilimia 39, Ofisa Ardhi wa Serikali za Mtaa anayechukua rushwa ya Sh milioni 5 asilimia 51 na mwanasiasa mwandamizi wa Taifa aliyeiba Sh milioni 100 asilimia 49.

Kwa upande wa madai ya kashfa za rushwa za hivi karibuni, asilimia 84 ya wananchi wamesema serikali ilishughulikia kesi ya Acacia vizuri na wananchi asilimia 67 walisema kesi ya TRA ya ukwepaji kodi ilishughulikiwa vizuri, huku asilimia 38 wakisema kesi ya Escrow ilishughulikiwa vizuri.

Hata hivyo, alisema wananchi wapo tayari kujitolea ili kupunguza rushwa ambapo asilimia 81 walikubali kuwa ni muhimu kupambana na rushwa hata kama itachelewesha maendeleo wakati asilimia 19 wanasema kusiwe na ukali kwa kuwa itaathiri uchumi.