Wachimbaji wadogo 150 wavamia mgodi, mmoja afa

WALINZI wa Kampuni ya Zeneth wanaolinda mgodi wa almasi wa Williamson Diamond Limited uliopo Kata ya Mwadui Lohumbo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, wamevamiwa na wachimbaji wadogo maarufu kama Wabeshi zaidi ya 150 kwa kurushiwa mawe na kusababisha kifo cha mchimbaji mdogo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Simon Haule alithibitisha kutokea kwa tukio hilo Novemba 20, mwaka huu saa 5 usiku katika eneo la shimo namba nane ndani ya mgodi huo, ambako walinzi wa mgodi huo walianza majibizano na wachimbaji wadogo hao.

Kamanda Haule alisema Wabeshi zaidi ya 150 walivamia eneo la mgodi linalochimbwa na mgodi huo na kulindwa na walinzi kutoka Kampuni ya Zeneth, ambako walianza kurushiwa mawe na kusababisha kifo cha Gile Ikula (20), mkazi wa Kijiji cha Nyenze wilayani humo ambaye alikuwa miongoni mwa Wabeshi.

Hata hivyo, kamanda alisema watuhumiwa wawili ambao ni walinzi wanashikiliwa na Polisi kwa mahojiano zaidi ambao ni Fabian Bona (25) na Paschal Patrick (27), huku watuhumiwa wanne ambao ni Lucas Gilungile (24), Charles Kija (25), Joseph Tungu (28) na Charles Mluso (32) wanashikiliwa kwa tuhuma za kuwajeruhi walinzi.

Alisema baada ya tukio hilo, baadhi ya Wabeshi waliubeba mwili wa marehemu na kuupeleka kwenye taa ya shimo namba nane, na tayari wanashikiliwa na Polisi kwa hatua zaidi za kisheria pamoja na kufanya mahojiano na watuhumiwa hao. Kamanda alitoa rai kwa wananchi hasa vijana kuacha tabia ya kuvamia maeneo ya migodini kwa lengo la kutafuta mchanga wa madini ya almasi kinyume cha sheria.