Tani milioni 2 za muhogo kuuzwa China

SERIKALI imesema iko kwenye mazungumzo na China ili kujua viwango vya muhogo vinavyohitajika ili kukidhi soko la zao hilo nchini humo. Akizungumza na Habari- Leo jana, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema kuna soko la tani milioni 2 za muhogo ya kutoka Tanzania nchini China.

Soko hilo kama litatumiwa vizuri na Watanzania, litaiingizia Taifa Dola za Marekani milioni 300 (Sh bilioni 670) na tani moja ya muhogo inauzwa kwa Dola za Marekani 150 ambayo ni zaidi ya Sh 300,000.

Mwijage alisema serikali iko kwenye mazungumzo na ubalozi wa China nchini ili kujua viwango (standards) vya muhogo vinavyotakiwa. Alisema China ni wakali kwenye suala la viwango na wako tayari kuitosa mihogo yote baharini kama watagundua kasoro hata, ikiwa ni ndogo.

Eneo ambalo serikali imepanga kwa uzalishaji mkubwa wa muhogo ni eneo la Ukanda wa Pwani hasa mikoa ya Lindi, Tanga, Mtwara na Mkoa wa Pwani. Waziri huyo alisema katika mikoa hiyo kipaumbele cha kwanza itakuwa Mkoa wa Lindi.

Alisema uzalishaji wa zao hilo nchini bado uko chini kwa sasa kwa kuwa hekta moja inatoa tani 3 ikilinganishwa na China ambako hekta moja inatoa tani 50. Alisema kwa Afrika Nigeria ndiyo inaongoza kwa kuuza tani milioni 44 za muhogo nchini China kwa mwaka.

Akihutubia kwenye sherehe za 68 za Siku ya Taifa la China zilizofanyika Septemba mwaka huu, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Susan Kolimba alisema Serikali ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China zilisaini makubaliano yaliyofungua masoko ya China kwa ajili ya muhogo mikavu kutoka nchini.

Dk Kolimba alisema kupitia makubaliano hayo, kumekuwa na mazungumzo kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Kichina ya Wuxi Goodways International Trade Co, Ltd (WGIT) kwa ajili ya kusafirisha mihogo kwenda China. Alisema kampuni hiyo ilipanga kuanza kusafirisha muhogo kutoka hapa nchini kabla ya mwaka huu kwisha