Abiria wa ndege washuhudia kombora la Korea Kaskazini

WIKI iliyopita Korea Kaskazini ilifanya jaribio la kombora la masafa marefu ambalo ilisema kuwa linaweza kufika popote nchini Marekani.

Kombora hilo mbali na kuzidisha uhasama na jirani zake pamoja na Marekani, pia lilizua tafrani kwa abiria waliokuwa katika ndege eneo la anga la Japan. Wahudumu wa ndege ya Shirika la Cathay Pacific iliyokuwa katika anga ya Japan waliripoti kuona Kombora la Korea Kaskazini lililokuwa likifanyiwa majaribio nchini humo.

Shirika hilo lilithibitishia BBC kuwa wahudumu wa ndege waliona kitu ambacho kilikisiwa kuwa kombora hilo likiingia kwenye anga ya dunia. Korea Kaskazini mara nyingi haitangazi pindi inapotaka kufanya majaribio ya makombora yake na wala haitoi tahadhari na hata njia mbayo hupitia mara nyingi haijulikani.

Hiyo ni kutokana na nchi hiyo kutokuwa na uwezo wa kupata data ya safari za angani ili ipate kuelewa kabla ya kufanya jaribio lolote la kombora. Kombora hilo lililotajwa kuwa lenye nguvu zaidi lilianguka katika maji ya Japan lakini japokuwa ndilo kombora lililopaa mbali zaidi kuliko kombora lolote lililofanyiwa majaribio na taifa hilo la Kikomunisti.

Jaribio hilo lilizua msukosuko zaidi kati ya Korea Kaskazini na majirani zake pamoja na Marekani, ambao Jumatatu walianzisha mazoezi yao makubwa zaidi ya angani kuwahi kufanywa, ambayo yametajwa na Korea Kaskazini kuwa uchokozi.