Benki ya Dunia yaahidi neema kwa Tanzania

MWAKILISHI wa Benki ya Dunia (WB) katika nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia, Bella Bird amemhakikishia Rais John Magufuli kuwa benki hiyo imejipanga kuendelea kutoa mikopo nafuu kwa miradi mbalimbali ya maendeleo ili kukuza uchumi na kupunguza umasikini Tanzania.

Bird alitoa kauli hiyo Ikulu jijini Dar es Salaam jana na kubainisha maeneo ya kipaumbele kuwa ni miundombinu, hususani barabara na reli, kuongeza uzalishaji na usambazaji wa nishati ya umeme, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) na elimu kwa kujielekeza katika ubora na kuhakikisha idadi ya wanaopata elimu inaongezeka.

Maeneo mengine ni kuboresha sekta ya afya, kuongeza upatikanaji wa maji, usimamizi bora wa ardhi, mawasiliano, huduma za fedha jumuishi, vituo vya pamoja vya Serikali na kusaidia familia masikini.

Pia Bird alimpongeza Rais Magufuli kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo, inayotekelezwa na Benki ya Dunia na alimuahidi kuwa benki hiyo itaendelea kushirikiana kwa karibu na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mingine.

“Mwaka uliopita Benki ya Dunia imetoa mikopo nafuu yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.2 (Sh trilioni 2.7) kwa Tanzania, fedha hizi zimekwenda katika miradi mbalimbali na tunafurahi kuwa miradi hiyo inakwenda vizuri na wananchi wanafurahia, kwa sasa tunapanga namna tutakavyotoa mikopo kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za maendeleo katika kipindi kijacho,” alisema Bird.

Kwa upande wake, Rais Magufuli aliishukuru Benki ya Dunia kwa ushirikiano wake na Tanzania katika maendeleo na alimhakikishia Bird kuwa Serikali itazisimamia vizuri fedha zote, zinazotolewa na benki hiyo ili zilete matokeo yanayotarajiwa.

Rais Magufuli aliongeza kuwa maeneo yote, ambayo benki hiyo imeyataja kuwa kipaumbele katika fedha zitakazotolewa, kuanzia sasa ni muhimu kwa ustawi wa Tanzania. Alisisitiza kuwa fedha zitakazotolewa kwa mkopo, zielekezwe katika maendeleo na siyo vinginevyo.

“Naishukuru sana Benki ya Dunia kwa kutuunga mkono, nitafurahi kuona mnaendelea kutupatia fedha ambazo zinaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo na kuleta manufaa mapana na endelevu, badala ya kugawa fedha kwa watu na baadaye nchi inakuja kuzilipa kwa kukusanya kodi za wananchi,” alisisitiza Rais Magufuli. Wakati huo huo, Rais Magufuli jana aliongoza kikao cha Baraza la Mawaziri, kilichofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.