Mambo 5 yabana shule binafsi, waomba mpango wa PPP kuziokoa

UBORESHAJI wa maeneo matano katika shule zinazomilikiwa na serikali nchini umebainika kuanza kuzitoa jasho shule za binafsi, hivyo kutishia ushindani wa shule hizo kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Maeneo ambayo yameanza kuboreshwa na kubainika kuleta uhai mpya kwa shule za serikali ni utekelezaji wa sera ya elimu bure, uboreshaji wa maslahi wa walimu, nidhamu ya walimu katika ufundishaji, ununuzi wa vitabu na zana za kufundishia na kujifunzia.

Hayo yalibainika Dar es Salaam jana wakati gazeti hili lilipofanya mahojiano maalumu na Katibu Mtendaji wa Shirikisho la Watoaji wa Elimu Wasiotegemea Serikali Kusini mwa Jangwa la Sahara (CIEPSSA), - Mbali ya Nkonya kusema kuwa hali hiyo imebadilika ghafla kutokana na kazi kubwa inayofanywa na serikali ya awamu ya tano ya Rais John Magufuli, ametabiri kuwa hali hiyo ikiachwa bila kuwekewa mkakati maalum itasababisha anguko kubwa kwa shule za binafsi.

Ili kuepukana na hali hiyo, shirikisho hilo limeiomba serikali kuweka mkakati wa kuziokoa shule hizo kwa kuziingiza katika utaratibu utakaoimarisha ushirikiano baina ya wamiliki wa shule za binafsi na serikali, ikiwemo walimu wa serikali kuruhusiwa pia kufundisha katika shule za binafsi.

Nkonya ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Sera na Majadiliano wa Shirikisho la Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi Tanzania (TAMONGSCO) alisema sababu ya kwanza inayozipaisha shule za serikali sasa ni kupanda kwa hali ya ufundishaji katika shule za serikali.

Alisema mkakati unaofanywa na serikali wa kufufua shule zake, lakini pia usimamizi wa karibu wa ufundishaji umegeuka kuwa kichocheo kikubwa cha kubadili mtazamo wa wazazi ambao sasa wameanza kupendelea watoto wao kusoma katika shule za serikali.

“Kwa kipindi cha hivi karibuni idadi ya wanafunzi katika shule zetu umeshuka kwa wastani wa asilimia 23, kuna kila dalili kuwa ifikapo mwanzoni mwa mwaka ujao kutakuwa na anguko kubwa mara tatu zaidi ya sasa,” alisisitiza Nkonya. Aliitaja sababu ya pili kuwa ni utekelezaji wa Sera ya Elimu Bure ambao umefanya wazazi wengi kupata mwamko wa kuwapeleka watoto wao katika shule za serikali kutokana na hatua hiyo kutowagharimu fedha yoyote.

“Unajua maisha ya ujanja ujanja hivi sasa hayapo tena kwa hiyo wazazi wengi hawana fedha za kuwasomesha wanafunzi katika shule za binafsi ambazo zinatoza ada kubwa. Hatua hii pia imeziathiri sana shule zetu,” alisema.

Alisema pia serikali imeanza mpango maalumu wa kupeleka mabilioni ya fedha ili kugharamia ununuzi wa vitabu vya kisasa vya ufundishaji hatua ambayo inazifanya shule za serikali kuwa na vitabu vya kutosha kama ilivyo kwa shule binafsi na hivyo elimu kuwa bora zaidi kuliko zamani.

“Mpango huu ni wazi utaziua zaidi shule ya binafsi, na ndio maana tunasema ni lazima nguvu ya ziada ifanywe ili kuziokoa shule hizi,” alisema. Aliitaja sababu ya nne kuwa ni hatua ya shule za serikali hasa kongwe kuanza kufundisha kwa mitaala inayotazamwa kwa karibu na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, hatua inayofanya elimu kuwa bora hivi sasa.

“Wengi tulianzisha shule zetu ili kufanyia kazi kasoro za utoaji wa elimu uliokuwepo katika shule za serikali ambazo hazipo tena tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli,” aliongeza Nkonya. Katika hatua nyingine, Nkonya alipongeza ufuatiliaji wa karibu wa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako katika uboreshaji wa sekta ya elimu akisema kumeleta nidhamu ya utendaji kwa wafanyakazi wa shule za serikali na hivyo kufanya elimu inayotolewa kuwa bora.