Wana CCM 20 wajitokeza kumrithi Nyalandu

Wanachama 20 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamechukua fomu za kugombea ubunge wa Jimbo la Singida Kaskazini kumrithi mbunge wa zamani, Lazaro Nyalandu aliyehamia Chadema.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani za chama hicho, aliyekuwa Msaidizi wa Nyalandu ambaye sasa ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Elia Digha amechukua fomu pia.

Wengine waliochukua ni Athuman Mungwe, Noel Alute, Japhet Mungwe, Haider Gulamali, Narumba Hanje, Edward Ihonde, Alex Lissu, Amos Makiya, Ramadhan Labitu, Sabasaba Manase, Justine Monko, Juma Mgoo, Antony Mburu, Aaron Mbogho na Fanuel Nyonyi.

Jimbo la Singida Kaskazini liko wazi tangu Oktoba mwaka huu, baada ya CCM kumfukuza uanachama Nyalandu ambaye alikimbilia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema Uchaguzi mdogo wa jimbo hilo utafanyika Januari 13, 2018, na leo saa 10 jioni ndiyo mwisho wanachama wa CCM kuchukua fomu.

Mbali ya Jimbo la Singida Kaskazini, Januari 13, 2018, pia kutafanyika uchaguzi majimbo ya Longido, Arusha ambako Onesmo ole Nangole (Chadema) alivuliwa ubunge na Mahakama Kuu, na Songea Mjini, Ruvuma ambako mbunge wake, Leonidas Gama (CCM) amefariki.