FFU mwizi wa silaha Tabora jela miaka 15

MAHAKAMA mkoani Tabora imemhukumu Mkuu wa kikosi cha kutuliza ghasia mkoani Tabora ASP Bhoke Jullius Bruno na wenzake saba kwenda jela miaka 15 baada ya kupatikana na hatia kwa makosa matatu yaliyokuwa yakiwakabili ya kupanga njama ,kuiba silaha (bunduki 8 aina ya SMG na kushindwa kuzuia wizi huo .

Bhoke na wenzake CPL Idd Abdalah, PC Mwinyi Gonga na Said Mgonela aliyekuwa muhudumu waliokuwa wajiriwa wa jeshi la polisi upande wa kikosi cha kutuliza ghasia walikuwa wanakabiliwa na tuhuma tatu ikiwemo ya wizi wa bunduki nane aina ya SMG mali ya mwajiri wake.

Wengine waliopewa adhabu hiyo na Kaimu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Sharmira Sarwatt ambaye alisikiliza shauri hilo ni Shaban Haruna, Shaban Kabanika na Idd Supu. Akitoa hukumu hiyo Sarwatt alisema kuwa ni maoni ya mahakama hiyo kwamba upande wa Jamhuri umethibitisha pasiposhaka makosa hayo na inawatia hatiani washitakiwa saba kati ya kumi.

Sarwatt alisema katika hukumu hiyo kuwa ushahidi umeonyesha kuwa mshitakiwa wa kwanza hadi wa tatu ambao walikuwa ni waajiriwa wa jeshi la polisi walihusika katika makosa yote matatu ya kula njama, kuiba na kushindwa kuzuia tukio.

Aliongeza kuwa hakuna ubishi kwamba silaha hizo zilipotea, zilikuwa zikitunzwa ghalani, kibali kiliombwa kwa ajili ya kwenda kuzifanyia matengenezo na kwamba mbili kati ya hizo zilipatikana moja Mbagala na nyingine Sikonge.

Alisema kuwa kuiba silaha za jeshi ambazo zingetumika kulinda raia na mali zake si kitendo ambacho mahakama inakifuraia. Aliongeza kuwa mahakama imechukulia uzito wa makosa ya wizi wa silaha za jeshi hivyo inajukumu la kutoa adhabu kali kwa washitakiwa ili liwe funzo kwao na kwa jamii yenye tabia kama hizo ndipo akawahukumu kwenda jela miaka mitano kwa kila kosa.

Awali upande wa serikali ukiongozwa na wakili mwandamizi Juma Masanja aliiambia mahakama hiyo kuwa watuhumiwa hao walitenda makosa hayo kati ya mwezi Aprili 2013 na April 2014.

Ilidaiwa katika shitaka la kwanza kuwa katika tarehe tofauti washitakiwa walikula njama ya kuiba bunduki aina ya SMG mahali ambapo zilikuwa zimehifadhiwa katika ghala la kituo cha kutuliza ghasia cha mjini Tabora.

Upande wa mashitaka ulidai katika shitaka la pili kuwa katika kipindi hicho washitakiwa kwa pamoja bila kuwa na haki ya kuchukua silaha kwenye kituo cha FFU Tabora waliiba bunduki nane aina ya SMG.

Wakili Masanja alidai kuwa watuhumiwa wakiwa watumishi FFU Tabora walishindwa kutumia njia za kiusalama katika utunzaji wa silaha matokeo yake bunduki nane aina ya SMG ziliingia katika mikono ya watu wasioaminiwa na serikali.

Washitakiwa wengine watatu ambao walioachiliwa na mahakama baada ya kukoseka ushahidi wa kuwatia hatiani ni Charles Abiud, Emanuel Festo na Nicholaus Mlelwa. Upande wa utetezi katika shauri hilo namba 104/2015 uliwakilishwa na mwakili wasomi Kelvin Kayaga na Mussa Kassimu wote wa mjini hapa.