Gulamali ashinda kura za maoni ubunge Singida Kaskazini

Haider Gulamali ambaye ni mfanyabiashara mwenye asili ya Kiasia mjini Dodoma, ameibuka wa kwanza kwenye kura za maoni kugombea nafasi ya ubunge kwa tiketi ya CCM jimbo la Singida Kaskazini kwa kupata asilimia 60.

Gulamali aliwabwaga vibaya wagombea wengine 21 wa kinyang'anyiro hicho huku Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Singida, Elia Digha aliyedaiwa kuwa tishio akishindwa kurejesha fomu yake kwa muda uliopangwa, hivyo kujiondoa mwenyewe kwenye mpambano.

Kwa mujibu wa Msimamizi wa uchaguzi huo ambaye pia ni Katibu Mwenezi wa CCM mkoa wa Singida, Hamad Athumani, Gulamali alijikusanyia kura 606 kati ya kura halali 1,009 zilizopigwa.

Justine Monko ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji katika Halmashauri ya Liwale mkoani Lindi alichukua nafasi ya pili baada ya kujipatia kura 133 huku aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Huduma za Misitu Nchini, Juma Mgoo akiambulia kura 46 na Sabasaba Manase kura 39.

Katika mchakato huo wa kura za maoni, Aaron Mbogho ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro aliambulia kura tatu tu. Jimbo la Singida Kaskazini limekuwa wazi tangu Oktoba mwaka huu baada ya aliyekuwa Mbunge wake, Lazaro Nyalandu kukosa sifa kufuatia kufukuzwa uanachama wa CCM kwa kitendo chake cha kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).