Mkurugenzi atakayesajili 'makanjanja' TASAF kukiona

WAZIRI wa Utumishi na Utawala Bora, George Mkuchika amewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuwafukuza kazi mara moja waratibu wa TASAF watakaobainika kusajili watu wasiostahili kuingizwa kwenye awamu ya tatu ya Mpango wa Kuzinusuru kaya maskini kabla yeye hajafanya ziara ya kutembelea katika maeneo husika.

Ametoa agizo hilo leo jijini Tanga wakati wa ziara yake ya siku moja iliyolenga kuelewa shughuli za TASAF pamoja na kutembela chuo cha Utumishi wa Umma na kusema kuanzia sasa mkoa atakaoenda na kukuta tatizo hilo linaendelea hatasita kuamchukulia hatua Mkurugenzi mtendaji kwa kushindwa kuwajibisha wahusika.

Amesema kitendo kinachofanywa na waratibu hao katika baadhi ya halmashauri cha kusajili watu wenye afya njema na akili timamu na kuwaacha walengwa wakiwemo wazee hakiivumiliki katika utawala wa awamu ya tano kwakuwa kinalenga kuiharibia serikali na kuvuruga malengo ya utekelzaji wa mpango huo.