UN, Kenya walaani mauaji askari JWTZ

RAIS wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres wamelaani mauaji ya askari 14 wa Tanzania waliokuwa sehemu ya jeshi la UN la kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo (DRC).

Kenyatta amesema Kenya ambayo ni sehemu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kama zilivyo nchini nyingine za Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini, itaendelea kushirikiana na Tanzania kuimarisha amani ya DRC na eneo la maziwa makuu kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Kimkakati cha Rais (PSCU) kwenye barua aliyoiandika kwenda kwa Rais John Magufuli, Rais Kenyatta amesema, shambulizi dhidi ya askari hao waliokuwa DRC kwa ajili ya kuwezesha kupatikana amani ya kudumu ni la kinyama.

Desemba 7, mwaka huu jioni, waasi wa kundi la Allied Democratic Forces (ADF) walivamia sehemu ya Kikosi cha askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kilichopo DRC kulinda amani wakiwa ni sehemu ya vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataida nchini DRC (MONUSCO).

Shambulizi hilo lilifanywa kwenye kambi ndogo iliyopo eneo la Daraja Mto Simulike, barabara ya kutoka Oicha kwenda Kamango mpakani mwa Uganda Kaskazini, Mashariki mwa Wilaya ya Beni, Jimbo la Kivu Kaskazini.

Shambulizi hilo la kuvizia lilizusha mapigano baina ya kikosi cha JWTZ na waasi hao. Rais Kenyatta alitoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao na amewatakia heri waliojeruhiwa waweze kupona haraka.

Inadaiwa kuwa, wapiganaji wa kundi la waasi la ADF liliwashambulia askari hao kwa kushtukiza kilomita 70 nje ya mji wa Beni uliopo mashariki ya DRC. Kwa mujibu wa Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali James Mwakibolwa, shambulizi la Desemba 7, ni baya na halijawahi kutokea tangu vikosi vya jeshi hilo vianze kushiriki ulinzi wa amani DRC mwaka 2011.

Luteni Jenerali Mwakibolwa alisema mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam kuwa, shambulizi hilo lilidumu kwa saa 13, JWTZ likapoteza askari 14, wengine 44 wamejeruhiwa, na wawili hawajulikani walipo.

Rais Kenyatta amesema, Kenya itaendelea kushirikiana na Tanzania kuimarisha amani ya DRC na eneo la maziwa makuu kwa ujumla. Kwa mujibu wa kiongozi huyo, Serikali ya nchi hiyo na Wakenya watashirikiana na Serikali ya Tanzania na Watanzania katika kupata ustawi wa baadaye wa eneo hilo kwa njia ya amani.

Alisema, Kenya inatambua mchango muhimu wa askari wa kulinda amani na imekuwa ikishiriki mara nyingi kwenye kazi hiyo. Katibu Mkuu UN Naye Katibu Mkuu wa UN, Guterres amesema, shambulizi hilo halikubaliki na ni uhalifu wa kivita. “Nalaani vikali hili shambulizi.

Mashambulizi haya ya kudhamiria dhidi ya walinzi wa amani wa UN hayakubaliki na ni uhalifu wa kivita,” alisema Guterres kwenye taarifa yake. Kwenye ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii wa twitter, Guterres amesema, shambulizi hilo limemuudhi na kumshtua, ni uhalifu wa kivita na kusiwe na kinga kwa wahusika.

Katika ukurasa huo kiongozi huyo wa UN amesema kushambuliwa kwa walinzi wa amani DRC kumemuumiza kwa kuwa, wamekuwa wakihatarisha maisha yao kila siku kwa ajili ya amani na kulinda raia.

Kwa mujibu wa Guterres shambulizi hilo ni baya zaidi kwa walinzi wa amani wa UN katika miaka ya karibuni. Taarifa ya kiongozi huyo imesema, takribani askari watano wa DRC walikufa kwenye shambulizi hilo.

Akaziagiza mamlaka za nchi hiyo zichunguze tukio hilo na haraka ziwachukulie hatua za kisheria wahusika. “Kusiwe na kinga kwa mashambulizi kama hayo, hapa au kwingineko,” alisema Guterres.

Oktoba mwaka huu, wapiganaji wa ADF walituhumiwa kuwashambulia walinzi wa amani wa UN mashariki ya DRC, wakafa askari wawili, na wengine 12 walijeruhiwa. Tangu Oktoba mwaka 2014 waasi hao wanadaiwa kuua zaidi ya watu 700 kwenye mkoa wa Beni.

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa UN anayeshughulikia ulinzi wa amani, Jean – Pierre Lacroix amesema shambulizi hilo ambalo ni miongoni mwa mashambulizi mabaya zaidi kwa walinzi wa amani wa UN limemhuzunisha na kumchukiza.

Ameandika kwenye ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa twitter kuwa, wanatoa heshima kwa wapiganaji hao wa MONUSCO, wanatoa pole kwa familia za marehemu na wanashukuru kwa huduma yao na kujitoa kwao.

Kwa mujibu wa Lacroix, UN ina walinzi wa amani zaidi ya 112,000 wanawake na wanaume wanaofanya kazi ili wengine wawe na maisha mazuri. Luteni Jenerali James Mwakibolwa alisema shambulizi la DRC limeleta madhara makubwa lakini kikosi kilichopo huko bado kina uwezo wa kutekeleza majukumu kwa uhodari, ushupavu, weledi na umahiri.

“Ni bahati mbaya mashujaa wetu wameuawa wakiwa wanatekeleza jukumu la ulinzi wa amani nchini DRC, Tutawakumbuka daima mashujaa wetu hao,” alisema. Alisema taratibu za kusafirisha miili ya marehemu kuirejesha nchini zimefanyika chini ya utaratibu wa Serikali na UN.

Alisema kutokana na shambulizi hilo, JWTZ na Serikali wanaendelea kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kufanya uchunguzi katika eneo husika. “Kwa umoja wetu Watanzania tuombee dua roho za mashujaa wetu zipumzike kwa amani na majeruhi wetu wapone haraka iwezekanavyo ili warejee kutekeleza majukumu yao,” alisema Mwakibolwa.