Serikali yaunda Kamati ya utambulisho wa Tanzania katika utalii

SERIKALI kupitia Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangala imeunda kamati maalum ya watu waliobobea katika mambo ya ubunifu wa mikakati ya masoko, mawasiliano, mahusiano kwa umma, utalii na biashara.

Kigwangala katika taarifa yake aliyoituma hii leo kwa vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, amesema lengo kuu la kamati hiyo ni kuanzisha mchakato wa kitaalam (technical) wa kuandaa utambulisho mpya wa Tanzania kwenye masoko ya kimataifa ya Utalii.

Amesema kuwa Kamati hiyo inakusudiwa kufanya uchambuzi wa kina wa tafiti mbalimbali na kukusanya maoni kutoka kwa wadau muhimu kisha kuzipeleka kwake mapendekezo yao.

“Kamati hii inakusudiwa kufanya uchambuzi wa kina wa tafiti mbalimbali na kukusanya maoni kwa wadau mbalimbali muhimu kisha kuniletea mapendekezo yao,”alisema Kigwangala.

Aidha amesema kuwa licha ya kuwa Malisili na Utalii sio Wizara ya Muungano lakini masula ya Utalii kwa pande mbili za Tanzania Bara na Zanzibar ni vitu ambavyo katika utekelezaji haviwezi kukwepana na huchangia kudumisha muungano huo, hivyo Kamati inahusisha pia wajumbe kutoka Zanzibar.

“Maliasili na Utalii siyo Wizara ya Muungano na kwamba utalii, kimsingi ni katika mambo yatakayodumisha zaidi Muungano wetu na Umoja wetu, sababu kimkakati na kiutekelezaji hatuwezi kukwepana, na kwamba uuuzaji wa vivutio vya utalii ni katika mambo ya kufanywa kwa pamoja ili kuwa na tija kwa Taifa letu,” amesema Kigwangala.

Amesema kuwa alipokea ushauri kwamba ni vema toka hatua za awali kamati hiyo kuweka wajumbe wa kutoka serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwenye Kamati hiyo.

“Awali tulikuwa na fikra kwamba baada ya kazi za mwanzo kufanyika na kuwa na andiko la kitaalamu la kufanyia kazi, tungeanzisha mawasiliano rasmi ndani ya Serikali zetu mbili, ambapo kungekuwa na majadiliano ngazi ya wataalam na baada ya hapo ngazi ya Mawaziri,” amesema Kigwangala na kuongeza kuwa bado wa nampango wa kufanya hivyo.

Utamaduni uliojengeka wa kufanya kzi kwa pamoja kwa ukaribu kwenye kutangaza vivutio vilivyopo sehemu zote mbili za Muungano utaendelea kufanyika hivyo kwani watalii wanaokuja kwenye mbuga hupenda kwenda Zanzibar kufanya utalii wa fukwe na wa kiutamaduni, na wale wanaofika Zanzibar nao hutaka kuja Tanzania bara kutembelea vivutio vingine vya utalii.

Amesema yeye binafsi ni muumini mkubwa na mahiri wa Muungano, na utangamano kwa ujumla wake na ushirikishwaji kama zana muhimu ya kufanyia maamuzi nyeti, hivyo hawezi kuwa wa kwanza kukiuka msingi wa imani yake kama kiongozi.

Hivyo amesema pindi hatua stahiki zitakapofikiwa atakaa na Waziri mwenzake wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kushauriana na kukubaliana.