Rais Magufuli awarejeshea wakazi Dodoma ekari 129

RAIS John Magufuli amerudisha kwa wananchi ekari 129 za ardhi zilizochukuliwa na serikali kwa ajili ya kutumika kuzikia viongozi wakuu wa nchi.

Aidha, ametaka taasisi au mashirika ambayo yanataka kuchukua eneo hilo, wahakikishe wanawalipa fidia wananchi waliopo na kuagiza wananchi hao waipe thamani ardhi hiyo. Akizungumza wakati wa uzinduzi wa nyumba 150 zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Iyumbu, Dodoma, Rais Magufuli alisema kuwa sheria ya kutaka kutengwa kwa eneo kwa ajili ya kuzikia viongozi wakuu, ilipitishwa wakati akiwa Waziri.

Alisema kuwa alipanga endapo akifa akazikwe nyumbani kwao Chato na sio Dodoma na kwamba hakutarajia kwamba angekuwa Rais. ‘’Baada ya kuwa Rais, ndio nimeona hii sheria inapaswa kubadilishwa, kwa kuwa nilizungumza na kiongozi mmoja kuhusu suala hili la kuzikwa hapa Dodoma naye amekataa, hivyo nataka sheria hii ibadilishwe na wananchi warudishiwe ardhi yao,’’ alifafanua.

Hatua hiyo imekuja baada ya Mbunge wa Dodoma, Anthony Mavunde kuomba ardhi hiyo, ambayo serikali iliichukua kwa lengo la kuzikia wananchi, irudishwe kwa wananchi kwani hakuna fidia yoyote, ambayo serikali imelipa na eneo halifanyiwi kitu chochote. Rais Magufuli alisema kuwa ni lazima wananchi warudishiwe ardhi yao na waiendeleze, kwa kuwa thamani yake imepanda ambapo wanaweza kufaidika nayo.

‘’Shirika linalotaka kuchukua ardhi hii wawalipe fidia wananchi hawa…tena nawaomba msiondoke katika maeneo yenu hadi mlipwe…hata kesho limeni, pandeni komamanga, mipapai kuipa thamani ardhi yenu,’’ alisisitiza. Pia alisema kwa kuanzia leo wananchi wowote watakaohitaji kuuziwa ardhi, wawapatie kwa kuwauzia vipande vipande, iwe wenyeji wa mkoa huo au hata kutoka mikoani.

‘’Mgogo akija mkatieni vipande vipande muuzieni, mkimuona Mzaramo amekaa vibaya muuzieni ardhi hii, lakini akija Msukuma mpeni bure…ninyi ni watani zangu, hivyo nataka mfaidike na ardhi hii,’’ alisema Rais Magufuli.

Aidha, alisema kuwa nyumba hizo zilizojengwa kwa kiwango cha juu na NHC, wapewe Idara ya Uhamiaji ili wafanyakazi wake waishi, zisikae bure na kwamba serikali itaendelea kufanya hivyo kwa jeshi la polisi na magereza. Alipongeza idara hiyo ya Uhamiaji kwa kazi nzuri wanayoifanya kukamata wahamiaji, tofauti na miaka ya nyuma na kuwataka kuendelea kutimiza wajibu wao ipasavyo.

Aliongeza kuwa NHC iwaambie mkopo wa Sh bilioni 200 wanaotaka, watarudisha kwa namna gani bila kuhusisha serikali. Wakati huo huo, Rais Magufuli aliwataka wakazi wa Dodoma kutumia fursa iliyopo katika kujiingizia mapato, ambapo tayari watumishi 3,000 wameshahamia jijini humo. Alisema kuwa kumekuwa na mikutano mbalimbali ya chama na taasisi inayoendelea kufanyika jijini humo, ambapo watu wengi wanatafuta mahali pa kulala na kuamua kulala Singida wakati wangeweza kulala Dodoma.

‘’Muache majungu na kambi sijui za Malecela, mara nani, ili kuleta maendeleo, hii ni nafasi pekee ya kutangaza mkoa na kutengeneza maisha yenu na nimefanya makusudi kumleta Mkuu wa Mkoa huyu ili kuleta maendeleo,’’ alisema Rais Magufuli na kuongeza; ‘’Kama leo (kesho) kutakuwa na mkutano wa walimu wote Tanzania watahitaji vyumba vya kulala, lakini inashangaza kuona hakuna gesti za kutosha za kulala hawa watu. Mtumie fursa hii vizuri na viongozi wenu kufaidika kiuchumi,’’ alisema.