Saida Karoli azisadia shule 5 za Ilala vitabu

Kampuni ya Big Entertaintment inayomsimamia msanii maarufu Saida Karoli imetoa vitabu mbalimbali vitakavyosambazwa katika shule tano za msingi zilizopoTabata wilayani Ilala, Dar es Salaam.

Kampuni hiyo itashirikiana na taasisi ya 'Bantu Digital Publishers’ inayojishughulisha na masuala ya uchapishaji vitabu kutekeleza mpango huo. Akizungumzia hatua hiyo Mratibu mpango huo, Amon Katagira alisema hatua hiyo imelenga kuunga mkono juhudi za Serikali za kuziwezesha shule mbalimbali za serikali na watu binafsi katika utoaji wa elimu bora ili kukuza viwango vya shule hizo na zingine nchini.

Amon alisema kutokana na umuhimu wa suala la elimu, Bantu Publishers na Big Entertainment kwa pamoja ziliona vyema kuunganisha nguvu zao na kukusanya vitabu hivyo maalumu kwa ajili ya wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la saba ili viweze kusaidia katika ufundishaji.

Alisema vitabu hivyo vyenye mtaala wa ufundishaji uliopendekezwa matumizi yake na Serikali, kwa kiasi fulani utakuwa msaada kwa wanafunzi katika shule hizo za Serikali na binafsi zikiwemo za Macedonia na Genius, zote kutoka Tabata katika manispaa ya Ilala.

Alisema vitabu hivyo vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni mbili, wanaamini vitakuwa chachu ya wanafunzi wote kusoma kwa bidii pamoja na jamii nzima kutambua umuhimu wa suala la elimu hivyo nao kujitolea katika kuchangia.