Mbunge Chadema amfuata JPM

MBUNGE mwingine kutoka vyama vya upinzani, amejivua uanachama na kujiuzulu ubunge kuanzia jana ili kumuunga mkono Rais John Magufuli kwa utendaji wake mzuri.

Mwingine aliyeondoka hivi karibuni ni wa Chama cha Wananchi (CUF) jimbo la Kinondoni, Maulid Mtulia. Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Mbunge wa Jimbo la Siha mkoani Kilimanjaro kwa tiketi ya Chadema, Godwin Mollel alisema kuwa uamuzi huo ni wake mwenyewe, ameufanya akiwa na akili timamu na hajashinikizwa na mtu yeyote.

Alisema kutokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya uongozi wa Rais Magufuli kupigania rasilimali za nchi, amejikuta dhamira yake ikishindwa kuvumilia na hivyo kuamua kujivua uanachama wa Chadema pamoja na ubunge ili aungane na CCM kwa ajili ya kutekeleza jukumu hilo muhimu kwa Taifa.

“Dhamira yangu imeshindwa kuukataa ukweli huu kuwa hivi sasa uongozi wa nchi yetu chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), umedhihirisha wazi kupigania rasilimali za nchi yetu,” ilieleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mollel alisema kuwa pamoja na kupiga hatua za kimaendeleo jimboni kwake ikiwemo ujenzi wa barabara, daraja, hospitali na miundombinu mbalimbali, hatua aliyoichukua inalenga kukamilisha dhamira ya kupigania rasilimali za Taifa akiwa CCM.

Aidha, Mollel aliwashukuru wananchi wa Jimbo la Siha kwa kumwamini na kumchagua kuwa mbunge wao katika uchaguzi mkuu uliopita pamoja na ushirikiano waliompatia kwa kipindi hicho cha miaka miwili ya ubunge wake.

Mbali na kuwashukuru wananchi, Mollel pia aliwashukuru viongozi wote alioshirikiana nao mpaka hatua aliyofikia na kuwaomba viongozi hao waendelee kushirikiana naye katika ujenzi wa Taifa.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Tanzania Bara, John Mnyika alipoulizwa kuhusu kujiuzulu kwa Mbunge huyo alisema wao kama chama hawajapokea taarifa rasmi za kujiuzulu kwa mbunge huyo.

Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai alisema kuwa hana taarifa yoyote ya mbunge huyo kujiuzulu. “Ndio kwanza nasikia kwako, sina taarifa yoyote ya kujiuzulu kwa mbunge huyo,”alieleza Kagaigai.

Kwa upande wake, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alithibitisha kupokewa kwa barua ya Mollel ya kutaka kujiunga na chama hicho.

Polepole alisema jambo hilo lilifanyika jana katika ngazi ya wilaya mkoani humo na kuongeza kuwa anachokifanya Mollel ni kurudi CCM, kwa kuwa awali alikuwa mwanachama wao. Kwa mujibu wa Polepole, taratibu nyingine ndani ya chama zinaendelea ili kukamilisha jambo hilo lakini pia alimpongeza Mbunge huyo kwa hatua aliyoichukua.