Ndege zisizo rubani kupeleka dawa visiwani

HUDUMA za matibabu kwenye vituo vya afya vilivyopo visiwani katika Ziwa Victoria mkoani Mwanza zinatarajiwa kuboreshwa baada ya kubuniwa ndege zisizo na rubani zitakazokuwa zinapeleka vifaa tiba na dawa.

Akizungumza katika uzinduzi wa mpango huo jijini hapa juzi, Mtaalamu wa Mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTEC), George Mulamula alisema mkoa wa Mwanza umeteuliwa kuwa kituo cha kijiografia cha ubunifu wa ndege hizo.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Leonard Subi alisema teknolojia hiyo itasaidia kuokoa maisha kwa kurahisisha huduma za matibabu kwa wakazi wa visiwa mbalimbali na kwamba Ukerewe kitakuwa cha kwanza kunufaika na huduma ya ndege hizo.

“Huduma za chanjo, dawa na nyinginezo za afya, hata za kusafirisha sampuli zinahitaji kuwa na uharaka wa aina yake. Kwa hiyo hii ni fursa kwa mkoa wetu wa Mwanza kwa sababu utakuwa ni mkoa wa kwanza Tanzania kutekeleza jambo hili na hii teknolojia imekuja wakati mwafaka,” alisema.

Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Bohari ya Dawa (MSD) nchini, Laurean Rugambwa alisema ndege hizo zitakakuwa na uwezo wa kubeba vifaa tiba na dawa hadi zenye uzito wa kilo nne, hivyo zitapunguza gharama ya uendeshaji wa bohari hiyo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella alisema ndege hizo zitakuwa mkombozi wa wakazi wa visiwa ambavyo ni vigumu kufikika, wanaohitaji huduma za dharura katika vituo vya afya.