Reli ya Tanga-Arusha iliyokufa miaka 14 yafufuliwa

SERIKALI imesema imeanza kufufua reli ya kaskazini ya kutoka Tanga hadi Arusha, ambayo ilikufa miaka 14 iliyopita.

Lengo la hatua hiyo ni kuwezesha wafanyabiashara na wananchi, kusafirisha mizigo yao kwa kutumia reli hiyo badala ya barabara, hatua itakayopunguza uharibifu wa miundombinu ya barabara nchini.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alipokuwa akikagua ukarabati wa reli hiyo kuanzia eneo la Korogwe hadi Mombo, ambalo limekamilika kwa kilometa 83.

Aliwahakikishia Watanzania kuwa uendelezaji wa reli hiyo hadi Arusha, utakamilika Aprili mwakani, hivyo kuruhusu huduma za usafirishaji ziendelee hasa za mazao na bidhaa. “Niwahakikishie wananchi kuwa hii kazi tuliyoianza haiwezi kusimama kwani serikali imejipanga na itaendelea kuhakikisha wananchi wanapata huduma nzuri za usafirishaji,” alisema Mbarawa.

Alimtaka Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO), Masanja Kadogosa, kuongeza ajira kwa vijana wa maeneo hayo. Aliwataka kuwa na uzalendo katika ukarabati wa reli hiyo ili kurahisisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Kuhusu ‘bomoabomoa’ katika maeneo ya hifadhi ya reli, Profesa Mbarawa alisisitiza kuwa ataendelea kusimamia sheria kama inavyosema.

Aliutaka uongozi wa Shirika la Reli Tanzania (TRL), kutafuta mizigo ili kuongeza huduma za usafirishaji wa mizigo kwani ukarabati wa njia hizo za reli, unahitaji fedha nyingi, hivyo upatikanaji wa mizigo hiyo utasaidia kuzalisha faida ambayo itawezesha kuongeza mapato ya shirika hilo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO, Masanja Kadogosa, alisema kuwa ukarabati wa reli hiyo, utakuwa na mchango mkubwa kiuchumi na kijamii, kwani utasaidia kwa wananchi na wafanyabiashara kusafirisha mizigo yao kwa njia rahisi. Ukarabati wa reli hiyo yenye urefu wa kilometa 438 ni mkakati wa Serikali katika kufufua huduma za usafiri wa treni nchini na kufungua fursa za kiuchumi na kibiashara kwa wananchi.