Dk Mwakyembe ateta na Wadhibiti wa Maudhui ya Luninga

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ameagiza taasisi zote zinazohusika na udhibiti wa maudhui ya luninga nchini kubuni mkakati wa pamoja wa kuboresha udhibiti.

Dk Mwakyembe ametoa rai hiyo baada ya kuzikutanisha taasisi hizo za udhibiti leo jijini Dar Es Salaam. "Nyinyi nyote ni taasisi za Serikali, hivyo tengenezeni mkakati wa kufanya kazi kwa pamoja kudhibiti maudhui mabovu ili kulinda maadili ya jamii yetu," alisema.

Waziri Mwakyembe alifanya mkutano wa pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Bodi ya Filamu Tanzania (TFB) na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA). "Kuna hitaji za kuongeza uwezo wa kufuatilia maudhui ya luninga ikiwa ni pamoja na filamu zote ili kubaini maudhui hasi kwa jamii yetu na kuzishughulikia ipasavyo kabla hazijaleta madhara kwa jamii," alisema.

Alisema changamoto za ongezeko la mahitaji ya jamii zinazidi kukua kwa haraka kutokana na kasi ya maendeleo hivyo ni vizuri kuhakikisha kuwa majawabu yake yanapatikana. Hata hivyo aliema kuwa Wizara yake haizuii maendeleo ya sanaa nchini ambayo inapiga hatua kwa kasi bali ni vizuri pia sheria za nchi zikazingatiwa ili kufikia maendeleo tunayohitaji.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bi Susan Mlawi, alisema Wizara itaangalia jinsi ya kuunganisha majukumu ya taasisi zinazosimamia maudhui ya vyombo vya utangazaji nchini ili kuimarisha udhibiti wa pamoja.

Akimweleza Waziri Mwakyembe changamoto za udhibiti wa filamu zinazoingia nchini, Bi Joyce Fissoo, alisema filamu nyingi zinaingizwa nchini kwa njia ya mtandao. Bi Fissoo ambaye ni Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, alisema kila filmu inayoonyeshwa kwenye luninga, lazima iwe imehakikiwa na kupangiwa daraja kwa mujibu wa sheria.

Akiongea katika mkutano wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dodoma mapema wiki hii, Rais John Pombe Magufuli aliiagiza Wizara ya Habari na TCRA kutosita kuvichukulia hatua vyombo vya utangazaji zinavyokiuka kanuni za utangazaji nchini.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Godfrey Mngereza, alipendekeza mashairi ya nyimbo yapitie katika taasisi yake wakati picha jongevu zipelekwe katika Bodi ya Filamu Tanzania. Dk Mwakyembe alisisitiza kuwa maudhui yanayoshabikia ushoga na utupu yasipewe nafasi katika luninga na filamu.