Msekwa: Chaguzi ndogo ndiyo gharama ya demokrasia

SPIKA mstaafu wa Bunge, Pius Msekwa amesema chaguzi ndogo zinazotarajiwa kufanywa kujaza nafasi za wazi za wabunge nchini baada ya wabunge kujiuzulu au kuhama vyama vyao si matumizi mabaya ya fedha za umma, bali ndio gharama ya demokrasia ya kweli katika nchi mbalimbali duniani.

Msekwa, ambaye ni Mwanasheria na Makamu Mwenyekiti wa zamani wa chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania bara, amesema hayo Dar es Salaam jana, alipoulizwa maoni yake kuhusu kufanyika kwa chaguzi ndogo katika majimbo kulikotangazwa na Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC).

Mwanasiasa huyo mkongwe anaungana na wasomi na wanasiasa wengine nchini, waliosema katika mahojiano tofauti jana kuwa, kitendo cha wabunge, madiwani na viongozi wengine wa kisiasa kuhama vyama vyao au kujiuzulu nyadhifa walizonazo ni haki yao ya kidemokrasia na hawapaswi kulaumiwa.

Wasomi na wanasiasa hao walisema hayo walipoulizwa maoni yao kuhusu mwenendo wa siasa nchini, kutokana na wimbi la wabunge na madiwani wa vyama vya upinzani kujiuzulu nyadhifa zao na kuhamia CCM na hivyo kufanya kufanyike chaguzi ndogo.

Wamesema, kufanyika kwa chaguzi hizo ni haki ya msingi ya kikatiba kwani Tanzania imeridhia mfumo wa kidemokrasia tangu mwaka 1992 na hivyo mbunge au diwani akifa, kujiuzulu au kuvuliwa uanachama, suala la kufanyika kwa uchaguzi mdogo haliepukiki hata kama ni gharama kufanya hivyo.

Walisema hayo wakati wakizungumzia kauli ya Mbunge wa Viti Maalumu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA), Upendo Peneza aliyewaambia waandishi wa habari jana kuwa, gharama za uchaguzi mdogo kwenye majimbo na kata ambako wabunge na madiwani wa vyama vya upinzani wamehamia vyama vingine ni matumizi mabaya ya kodi za wananchi, kwa kuwa ni gharama kubwa kuendesha chaguzi hizo ndogo kwa sasa.

Peneza alisema kuwa chaguzi hizo kwa ngazi ya jimbo hugharimu siyo chini ya Sh bilioni moja ambazo zingeweza kutumika katika mambo mengine. Alisema hayo akidai kukerwa na wimbi la wabunge na madiwani kujivua nyadhifa zao na uanachama wa vyama vyao na kujiunga na vyama vingine.

Alisema hatua ya wanasiasa hao inawaongezea mzigo wananchi kwa kuwa fedha zinazotumika kugharamia uchaguzi wa marudio ni kodi zao wanazolipa. Hoja hiyo ya Peneza aliyosema kuwa ni mawazo binafsi na kuwa hakutumwa na chama chake cha Chadema, imeungwa mkono na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino cha Mwanza (SAUT), Peter Mataba aliyesema ni vyema sheria ya uchaguzi ikafanyiwa mabadiliko ili mgombea aliyefuatia wakati wa uchaguzi mkuu, apitishwe na Tume ya Uchaguzi (NEC) kuchukua nafasi husika pasipo kuingia gharama ya kufanya uchaguzi tena kila nafasi inapotokea.

Hata hivyo, Msekwa aliipinga hoja hiyo ya gharama akisema kuwa ni haki ya kidemokrasia ya wananchi kuhama vyama na uchaguzi kurudiwa. Alisema wakati Watanzania wanachagua mfumo wa kidemokrasia hawakuwa wendawazimu kwa kuwa walijua fika kwamba demokrasia ni gharama na kuongeza kuwa kupinga watu wasihame vyama na uchaguzi kurudiwa kwenye mfumo wa kidemokrasia ni udikteta ambao watu wengine wamekuwa wakiupinga pia.

“Ukimpenda mwanamke wa Kimakonde, mpende na ndonya zake. Kama tumechagua demokrasia tukubali na gharama zake. Kwa mfano huwezi kuwaambia watu kwamba tufanye uchaguzi kila baada ya miaka 10 eti kwa sababu kufanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano ni gharama, demokrasia ni gharama, ukiikubali lazima ukubali na gharama zake,” alieleza Msekwa alipoulizwa maoni yake kuhusu kuhamahama kwa wanasiasa na madhara yake.

Kuhusu kufanyiwa mabadiliko ya sheria ya uchaguzi ili kusiwepo na chaguzi za marudio, Msekwa alisema hakuna haja kwa sababu huwezi kuwalazimisha watu kubaki kwenye vyama kwa kigezo cha kuepuka gharama na kuwa ndiyo maana hata Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu alipoondoka, CCM walimtakia safari njema kwa kuwa ametumia haki yake ya kidemokrasia. Kuondoka kwa Nyalandu kumeifanya NEC itangaze uchaguzi mdogo huko.

“Ni kweli gharama ipo, lakini kama ukiona demokrasia ni ghali jaribu udikteta. Kufanya uchaguzi mdogo ni utaratibu wetu wa kidemokrasia tuliokubaliana endapo mbunge au diwani amekufa, kujiuzulu au kuvuliwa uanachama, hayo ni matakwa ya sheria,” alieleza Mhadhari wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Benson Bana alipoulizwa maoni yake kuhusu suala hilo.

Msomi huyo alisema kama kuna watu wanaona sheria hiyo ya kufanyika uchaguzi mdogo kila nafasi inapotokea ni gharama, wanaweza kupeleka hoja bungeni au kufungua kesi mahakamani au kudai katiba ibadilishwe ili jambo hilo lisiwepo.

Naye aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha UPDP, Fahim Dovotwa alisema kuwa suala la kufanyika uchaguzi mdogo siyo jukumu la mbunge au diwani aliyehama, kujiuzulu au kuvuliwa uanachama, bali ni hoja ya Serikali na Tume ya Uchaguzi (NEC).

Alisema watu kuhama vyama ni haki yao na suala la kufanyika uchaguzi sasa au baadaye ni jukumu la Serikali na Tume. Wanasiasa hao wametoa maoni hayo wakati Spika wa Bunge, Job Ndugai akiwa ametangaza majimbo mawili ya Kinondoni na Siha kuwa yako wazi baada ya wabunge wa majimbo hayo, Maulid Mtulia (CUF) na Godwin Mollel (Chadema) kujivua uanachama na kufanya majimbo yaliyo wazi na yanatakiwa kufanya uchaguzi kuongezeka baada ya Mahakama Kuu kutengua ubunge wa jimbo la Longido na pia mbunge wa Songea mjini, Leonidas Gama kufariki hivi karibuni.

“Rasmi sasa jimbo la Siha mkoani Kilimanjaro na Kinondoni jijini Dar es Salaam yako wazi,” alisema Ndugai jana alipozungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa amepokea barua kutoka kwa wabunge hao, Mollel na Mtulia.

“Wamenitaarifu kwa barua wanajivua uanachama wa vyama vyao na wamejivua nafasi zao za ubunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” alifafanua Ndugai. Tangazo la Spika linakuja wakati vumbi likiwa halijatulia kwani Januari 13, mwakani, kutakuwa na mtifuano katika majimbo ya Singida Kaskazini kutokana na kujiondoa CCM kwa Lazaro Nyalandu, Songea Mjini kutokana na kifo cha Leonidas Gama wa CCM na Longido kutokana na kutenguliwa kwa ubunge wa Onesmo ole Nangole wa Chadema.

Spika Ndugai alisema kutokana na hatua walizochukua wabunge hao wawili, siyo wabunge tena kuanzia jana na kwamba sasa ni rasmi kuwa majimbo hayo mawili yako wazi; na amekwishaiarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili kuchukua hatua kadri ya sheria na taarifa kama tume. Peneza amelalamikia gharama hizo wakati Chadema ikiwa na historia ya kushiriki na wakati mwingine uchaguzi mdogo wa udiwani kwenye baadhi ya kata 43 uliofanyika Novemba 26 mwaka huu na chaguzi nyingine ndogo za ubunge zilizowaahi kufanyika nchini.

Miongoni mwa kata ambazo Chadema ilishiriki ni Kata ya Mamba wilayani Lushoto mkoani Tanga kiliposimamisha Jafari Ndege, Kata ya Majengo wilayani Lushoto walipomsimamisha Abdallah Maonga, Kata ya Bomambuzi mkoani Kilimanjaro walipomsimamisha Hedlack Minde na kwenye Kata ya Ibhigi-Rungwe wakikomsimamisha Lusubilo Simba.

Pia waliwahi kushiriki chaguzi ndogo za majimbo ya Tarime baada ya kifo cha Chacha Wangwe, Busanda ambako alishinda Lolensia Bukwimbwa wa CCM, Igunga ambako alishinda Dk Dalali Peter Kafumu na jimbo lingine aliloshinda mgombea wao, Dk Mbassa.

Peneza aliwataka wananchi wasiwachague wabunge na madiwani hao kama watarudi kugombea tena kupitia vyama vingine kwa kuwa waliondoka kwa hiari yao na hawakufukuzwa uanachama. alisema kama mbunge au diwani anafurahishwa na kazi nzuri ya Rais John Magufuli hana sababu ya kumuunga mkono kwa kuhama chama au kujiuzulu nafasi zake za uongozi, bali anaweza kusimama bungeni au mahali pengine na kumuunga mkono bila kuleta gharama kwa wananchi za kuhama chama. Matern Kyera, Dar na Sifa Lubasi, Dodoma