Mauzo ya ‘kifisadi’ ya ardhi ekari 1,756 yafutwa

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amefuta uamuzi wa viongozi wa vijiji vya Membe na Mlimwa, Kata ya Membe wilayani Chamwino, Dodoma ya kutoa ekari 1,756 za ardhi kwa mwekezaji.

Vijiji hivyo vinadaiwa kutoa ardhi hiyo miaka 10 iliyopita na kusababisha migogoro mikubwa ya ardhi katika kata hiyo. Akizungumza na wakazi wa kata hiyo kwenye mkutano wa hadhara jana, Lukuvi alisema amefuta maamuzi yote yaliyofanywa na serikali za vijiji hivyo kwani yalikiuka Sheria ya Ardhi ya Vijiji Namba 5 ya Mwaka 1999 inayotoa mamlaka kwa vijiji kumilikisha ardhi isiyozidi ekari 50 tu na siyo vinginevyo.

“Kuanzia leo (jana) nimefuta maamuzi yote yaliyofanywa na viongozi wa vijiji hivi kumpa mwekezaji huyu ardhi yenye ukubwa wa ekari 1,756 kwani ni kinyume cha sheria ya vijiji,” alisema na kuongeza kuwa hata kama vijiji vitakubali kutoa ardhi kupitia mikutano mikuu ya vijiji bado maamuzi hayo hayatakuwa halali endapo ardhi inayotolewa itazidi ukubwa wa ekari 50.

Mwekezaji huyo, David Poli alipewa ardhi takribani miaka 10 iliyopita, hali iliyosababisha mgogoro wa ardhi na kuhatarisha amani katika kata hiyo. Wakazi wa kata hiyo walisema licha ya kukataa kutoa ardhi yao kwa mwekezaji huyo kupitia mikutano mikuu ya vijiji, viongozi wao walimmilikisha mwekezaji huyo ardhi hiyo ikiwemo ekari 100 alizopewa na Kijiji cha Membe kwa makubaliano kuwa atawajengea Ofisi ya Serikali ya Kijiji ahadi ambayo hata hivyo hajaitekeleza.

Lukuvi alimtaka mwekezaji huyo ambaye alifika katika mkutano huo, kufuata taratibu za kumilikishwa ardhi inayozidi ukubwa wa ekari 50 endapo ana nia ya kuendelea kuwekeza katika kata hiyo.

Alisema taratibu zipo wazi za umiliki wa ardhi wa aina hiyo. Alimtaka kuomba ardhi katika vijiji hivyo na endapo vitaridhia, vitapendekeza kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kumilikisha ardhi inayozidi ekari 50 baada ya ardhi hiyo kuhama kutoka katika mamlaka ya vijiji.