HabariLeo lazinduliwa rasmi Rwanda

KAMPUNI ya Magazeti ya Serikali (TSN) imezindua rasmi usambazaji na uuzaji wa toleo maalum la Afrika Mashariki la gazeti la Habarileo nchini Rwanda, jana.

Gazeti hilo litakuwa linauzwa nchini humo leo, mahususi kwa kukuza na kuendeleza Kiswahili pamoja na kuimarisha mtangamano wa Afrika Mashariki. Uzinduzi huo ulifanywa na Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Ali Idi Siwa na kuhudhuriwa na baadhi ya wananchi wa Rwanda wakiwemo wasomi na wataalamu wa lugha ya Kiswahili, wanafunzi wa vyuo vikuu na Watanzania waishio Rwanda.

Balozi aliwataka wananchi waliohudhuria hafla hiyo kuwa mabalozi wazuri. Kwa upande wake, Mhariri Mtendaji wa TSN, Dk Jim Yonazi aliwaahidi wananchi wa Rwanda kwamba TSN itawaongoza katika safari ya kukuza na kuendeleza Kiswahili kupitia gazeti la Habarileo.