Bil 13.8/- zafidia kupisha Ikulu

SERIKALI imeanza kulipa fi dia kwa wananchi ambao maeneo yao yametwaliwa kwa ajili ya ujenzi wa Ikulu ya Rais pamoja na Mji wa Serikali wilayani Chamwino mkoani Dodoma.

Hayo yamebainishwa juzi wakati Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge alipotembelea Kata ya Chahwa, Mtaa wa Muungano ambako shughuli ya kulipa fidia wananchi wa kata hiyo imeanza.

Ulipaji fidia huo unafanywa na Wakala wa Majengo (TBA). Mkurugenzi wa Idara ya Miliki katika TBA ambaye ni msimamizi wa ulipaji fidia, Baltazar Kimangano alisema hadi sasa wameshapokea Sh bilioni 13.8 kwa ajili ya ulipaji wa fidia wa jedwali la kwanza na kwamba malipo mpaka sasa yamefikia asilimia 60.

Kimangano alisema kwamba baada ya kufanya shughuli ya utambuzi wa eneo linalohitajika kwa ajili ya upanuzi wa Ikulu, walibaini haja ya ekari 8,900. Akizungumzia haja ya wananchi kuelimishwa kuhusu malipo yao na kuepusha malalamiko, Dk Mahenge alimuagiza Kimangano kuwaelekeza watendaji katika dawati la kutoa fedha za fidia kutoa ufafanuzi wa majedwali ya ulipaji huo.

Aidha, alitaka kuwepo na daftari la maelekezo ya mali ya kila mtu anavyolipwa kwa mwenyekiti wa mtaa ili kila mtu ajue taarifa zake mapema kabla ya kuchukua hundi za malipo yake.

Pia alitaka malalamiko yote kushughulikiwa papo hapo kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano haihitaji kuchelewesha kushughulikia manung’uniko ya watu wake. “Toeni ufafanuzi wa majedwali, inapokuwa shida kiko kitabu cha malalamiko, na malalamiko hayo yafanyiwe kazi,” alisema Dk Mahenge.

Alisema amefika kijijini hapo kuona namna watu wanavyolipwa fidia ili kupisha ujenzi wa Ikulu hiyo tayari kwa ajili ya kumpokea Rais John Magufuli muda wowote kuanzia mwakani. Aidha, aliwataka wananchi kuwa wazi katika kushughulikia fidia zao na kudai ufafanuzi katika tukio lililofanyika ili wajiridhishe.

Akizungumza kuhusu eneo hilo, Kimangano alisema kwamba awali walilipa hundi 50 za thamani ya zaidi ya Sh milioni 275 na kubakiza hundi tano zenye jumla ya zaidi ya Sh milioni 20.

Alisema juzi hiyo walikuwa wanatarajia kulipa hundi 50 na zilizobaki zinatarajiwa kulipwa Jumatatu na Jumanne na kwamba awamu ya pili ya malipo wanatarajia kuanza Jumatano ijayo.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili baada ya kikao cha mkuu wa mkoa, walisema kwamba ipo haja ya kuwapo na ufafanuzi wa malipo ya pango, usumbufu, nauli, fidia ya nyumba na eneo.

Wakiomba wasiandikwe majina yao gazetini, walisema kwa sasa fidia ipo katika fungu moja bila maelezo yanayotoa ufafanuzi fedha ipi ni kwa ajili ya nini. Aidha, waliomba mipango ya ulipaji ifanywe kwa ustadi ili mtu mmoja amalize shughuli yake siku hiyo na si kwenda na kurudi kesho kutokana na watu wengine kuwa na maeneo zaidi ya moja.