Mukoba adakwa kwa miamala ya rushwa

TAASISI ya Kupambana na Kuzuia Rushwa Tanzania (Takukuru) inamshikilia aliyekuwa Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba kwa tuhuma za kujihusisha na rushwa katika uchaguzi wa viongozi wa chama hicho.

Msemaji wa Takukuru, Mussa Misalaba aliliambia gazeti dada na hili la Sunday News jana, kwamba Mukoba alikamatwa jana saa tatu asubuhi na maofisa uchunguzi wa taasisi hiyo kwenye viwanja vya Chimwaga ambako uchaguzi huo ulikuwa unaendelea.

Misalaba alidai kwamba Rais huyo wa zamani CWT alikuwa anajaribu kuwahonga wapiga kura. Hakutoa maelezo zaidi kuhusu suala hilo. “Tunaendelea na uchunguzi wa suala hili. Kwa sasa naweza kusema hivyo, tutatoa taarifa zaidi kuhusu suala hilo baadaye,” Misalaba alikaririwa na Sunday News.

Mukoba alichaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa CWT mwaka 2002 na mwaka 2007 alichaguliwa kuwa Rais wa chama hicho, kabla ya mwaka 2014, kuchaguliwa kuwa Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta). Alistaafu ualimu hivi karibuni.

Wajumbe wa CWT wako Makao Makuu ya Nchi Dodoma kwa ajili ya Mkutano Mkuu wao ambao pamoja na mambo mengine, unatarajiwa kuwachagua viongozi wake wakuu. Akifungua mkutano huo Alhamisi, Rais John Magufuli aliwakumbusha viongozi kuchagua viongozi waadilifu.

Alitaka pia CWT ijiepushe na vitendo vya rushwa katika uchaguzi. Alionya kuwa vyombo vya dola vipo macho, kufuatilia na kuchukua hatua dhidi ya wote wanaojihusisha na rushwa.

Aliahidi kuwachukulia hatua wagombea wanaojihusisha na rushwa, akisema walimu wanahitaji viongozi ambao wanataka kuwanufaisha wengi kuliko wao wenyewe. Aidha, Rais Magufuli aliwahakikishia walimu wote nchini kuwa serikali ipo tayari kulipa madeni ya walimu, baada ya madeni hayo kuhakikiwa.

Pamoja na kulipa madeni ya walimu, Rais Magufuli alisema serikali inawajali walimu na ipo tayari kuboresha maslahi yao na kuboresha mazingira ya kazi kulingana na uwezo wake. Aliwataka Watanzania wakiwemo walimu, kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa ili nchi iwe na fedha za kutosha kuongeza maslahi hayo.