Shaka hana shaka na ukaguaji mali za UVCCM

KAIMU Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Shaka Hamdu Shaka amesema atatekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Mwenyekiti mpya wa umoja huo, Kheir James ikiwemo uratibu, uhakiki na upitiaji mikataba ya mali, mikataba rasilimali na vitega uchumi vya jumuiya hiyo Tanzania Bara na Zanzibar.

Amesema tangu ateuliwe kuwa Kaimu Katibu Mkuu amefungua milango ya kukaguliwa hesabu na wakaguzi wa ndani pamoja na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, hivyo anajiamini na hana shaka katika kusimamia maslahi mapana ya jumuiya.

Shaka alitoa matamshi hayo juzi baada ya Mwenyekiti mpya wa UVCCM Taifa kutaka ofisi za mikoa za umoja huo kufanya uhakiki wa mali, vitega uchumi na rasilimali za jumuiya ili zitumika kwa faida na manufaa ya jumuiya.

Alisema hakuhitaji kigugumizi wala kupoteza muda katika utekelezaji huo kwani ni masuala ya msingi na yenye umuhimu kwa jumuiya ya vijana, ikiwa ni mkakati kabambe wa kufanya mageuzi ya kiutendaji, kimfumo na uwajibikaji utakaorudisha heshima ya jumuiya hiyo.