Sekondari za Milambo, Jangwani, Azania ‘zapigwa stop’ kufunguliwa

WIZARA ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, imesitisha kufunguliwa kwa shule kongwe tatu za Milambo, Jangwani na Azania, zilizokuwa zifunguliwe kesho na sasa zitafunguliwa Januari 22 mwaka huu, kutokana na ukarabati unaoendelea.

Aidha, ratiba za masomo katika shule hizo zitarekebishwa ili kwa wiki hizo mbili ziweze kufidiwa, hivyo katika utaratibu wa kawaida muda huo utafidiwa wakati wa likizo fupi na ndefu ya mwezi Julai.

Wizara imeagiza Wakala wa Majengo nchini (TBA), kutekeleza majukumu yake kulingana na mikataba waliyoingia na shule hizo, pamoja na ujenzi wa Kampasi ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas).

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Leonard Akwilapo alisema jana alipotembelea Shule ya Sekondari ya Wasichana Jangwani iliyopo jijini Dar es Salaam na kujionea hali halisi ya maendeleo ya ukarabati katika shule.

Alisema shule tisa zinaendelea kukarabatiwa chini ya usimamizi wa TBA, na zipo kwenye hatua mbalimbali za ukarabati. Alitaja shule hizo kuwa ni Jangwani, Azania, Kibaha, Kigoma, Tosamaganga, Malangali, Milambo, Minaki na Nangwazi. Kwamba Shule ya Songea Wasichana bado haijaanza kukarabatiwa.

“Kama mnavyotambua shule zetu zinafunguliwa kesho kutwa (kesho) Januari 8. Wizara baada ya kufanya tathmini ya kina imegundua kuwa kwenye shule zinazokarabatiwa na TBA kumekuwa na tatizo la ukamilishwaji wa miradi kulingana na muda uliopangwa. “Miradi yote iko nyuma ya ratiba.

Na mbaya zaidi ni kwamba baadhi ya shule haziko tayari kabisa kupokea wanafunzi na wakaendelea na masomo yao kwa ukamilifu kwa kuwa mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji hayajakamilika,” alisema.

Alisisitiza kuwa wizara kwa kushirikiana na serikali za mikoa na halmashauri husika, itafanya usimamizi wa karibu kuhakikisha kuwa shule hizo zinakamilika katika kipindi hiki cha wiki mbili.

“Tunaomba radhi kwa usumbufu wowote utakaojitokeza kwa wazazi ama walezi na wanafunzi wanaosoma na waliochaguliwa kujiunga katika kidato cha kwanza katika shule hizi. “Natumaini mnatambua nia njema ya serikali ya kutaka kuimarisha mazingira ya shule hizi ambazo zilikuwa zimechakaa sana,” alisema.

Akwilapo alisema pia ni matarajio yao kuwa kampasi hiyo, itachukua wanafunzi wa kwanza mwaka huu, hivyo anawaagiza TBA kuongeza juhudi pale Mlonganzila ili lengo hilo litimie. “Maelekezo ya waziri wangu Profesa Ndalichako ni kuhakikisha kuwa tunafanya usimamizi wa karibu ili miradi yote ya TBA ianze kwenda kulingana na mikataba.

Tutafanya hivyo wakati pia tunaanglia taratibu za kisheria ili kama kuna hatua zozote muafaka ziweze kuchukuliwa ili malengo yakamilike kulingana na matarajio,” alisema. Wizara hiyo imekuwa ikiendelea na programu ya ukarabati mkubwa wa shule kongwe za sekondari nchini, programu ambayo itahusisha jumla ya shule kongwe 89.

Alisema katika awamu hiyo ya kwanza, ambayo imetekelezwa kwa miaka miwili sasa, yaani mwaka wa fedha 2016/17 na 2017/18, jumla ya shule 46 kati ya 89 zipo kwenye mpango wa ukarabati huo.

Alitaja shule 10 za sekondari ambazo ni Mpwapwa, Musoma Ufundi, Mtwara Ufundi, Ifakara, Kantalamba, Tanga Ufundi, Ifunda Ufundi, Moshi Ufundi, Bwiru Wavulana na Kibiti, zinaendelea kukarabatiwa kwa usimamizi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST).

“MUST ni taasisi ya kielimu, kwa hiyo wamekuwa makini sana na ratiba za shule. Shule zote hizi ziko katika hatua za mwisho za ukarabati na wanafunzi wanaendelea na masomo kama kawaida.

Vile vile alisema Shule za Sekondari za Iyunga, Chidya, Tambaza, Zanaki na Kisutu zinakarabatiwa chini ya uongozi wa Shule na Bodi za Shule kwa Usimamizi wa Halmashauri za Wilaya zao. “Nazo pia ukarabati unaendelea vizuri sana,” alisema.

Katibu Mkuu huyo alisema shule ya sekondari ya Ndwika ambayo iko Wilaya ya Masasi, inajengwa upya chini ya Halmashauri baada ya taarifa ya wahandisi kubaini kuwa majengo yake hayawezi kufanyiwa ukarabati.

“Shule za Sekondari za Nyakato na Ihungo nazo pia zinajengwa upya kufuatia kuharibiwa vibaya na tetemeko la ardhi lililotokea katika mkoa wa Kagera mwezi Septemba 2016… na kwa upande wa shule ya Sekondari ya Rugambwa, hii zinajengwa nyumba nane za walimu ambazo zilibomoka kutokana na tetemeko hilo,” alisema.

Aliongeza kuwa, pia wizara hiyo kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), inakarabati shule za sekondari 17 ambazo ni Ilboru, Same, Pugu, Mwenge, Nganza, Mzumbe, Kilakala, Tabora Wavulana, Tabora Wasichana, Msalato, Dodoma, Ruvu, Korogwe, Bwiru Wasichana, Sengerema, Bihawana na Kondoa Wasichana.

Kwa mujibu wa Akwilapo, katika shule hizo mpaka sasa 10 zimeshakamilika na saba zinaanza kukarabatiwa hivi karibuni bila kuathiri masomo. Kwa upande wake Kaimu, Meneja wa TBA mkoa wa Dar es Salaam, Manasseh Shekalaghe alisema mazingira ya kazi ndiyo yaliyosababisha kuchelewa kukamilika kwa ukarabati huo.

Aliongeza kuwa shule hizo kongwe zenye miaka zaidi ya 89, kuna sehemu za mapaa yalikuwa yanavuja wakaambiwa wazibe, lakini kitaalamu walishauri yatolewe na kubadilishwa.

“Katika kubadilisha mfumo wa umeme, gharama zilizotolewa siyo halisi kulinganisha na gharama zenyewe,” alisema na kuongeza hivi sasa wameandaa mpango kazi utakaoongeza kasi ya ukarabati.

Mkurugenzi wa Mipango Wizara ya Elimu, Gerald Modi alisema gharama za ukarabati wa shule zote kongwe ni zaidi ya Sh bilioni 11 na zilizolipwa mpaka sasa ni zaidi ya Sh bilioni tatu.

Alisema Aprili mwaka jana, serikali ilitenga Sh bilioni 11 kwa ajili ya ukarabati wa shule 10, ambapo mkataba ulikuwa shule hizo zikamilike baada ya miezi sita. Kwa maana ya kwamba baada ya makubaliano ukarabati huo ulitakiwa ukamilike Septemba mwaka jana, lakini waliongeza muda hadi Desemba mwaka jana