Askari 20 wanyamapori kuhamishwa Kilombero

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla, amemwamuru Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa), Dk James Wakibara kuwahamisha askari wote 20 na viongozi wao wawili na waliopo kambi za Hifadhi ya Bonde la Kilombero mkoani Morogoro kutokana na kushindwa kuwajibika kikamilifu.

Ametaka atekeleze agizo hilo haraka, wapangiwe maeneo mengine ya kazi na kisha kuchukua wengine wapya wanaofikia 40, ambao wataleta ufanizi wa kazi kwa kusimamia shughuli za ulinzi kwenye wa bonde hilo. Aidha, amemtaka mtendaji huyo aanzishe kituo (post) katika maeneo, ambayo wananchi wamekuwa wakivamia.

Waziri huyo alitoa agizo hilo wakati wa majumuisho ya ziara yake ya siku mbili juzi, aliyoifanya katika wilaya ya Kilombero na Malinyi mkoani Morogoro na kukagua Bonde la Kilombero kwa kutumia ndege ndogo, ikiwemo baadhi ya vijiji na vitongoji ambavyo vimeanzishwa ndani ya Hifadhi ya Bonde hilo na Pori Tengefu ikiwemo kitongoji cha Mkocheni Kijiji cha Namwawala wilaya ya Kilombero Kijiji cha Ipera Asilia wilaya ya Malinyi.

Dk Kigwangalla aliagiza watu wote waliopo ndani ya ardhioevu katika hifadhi ya Bonde hilo, ambao wameweka makazi na kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji, waondolewe mara moja na watakaokaidi agizo hilo hatua za kisheria kupitia sheria zilizopo za uhifadhi na za mifugo ambayo inaekeza utaifishaji wa mifugo inayokutwa ndani ya hifadhi.

Hata hivyo, alisema baada ya kuondolewa kwa mifugo ndani ya hifadhi ya bonde hilo, sensa ifanyike sambamba na upigaji chapa mifugo ili kupata idadi kamili kwa wilaya za Kilombero, Malinyi na Ulanga ili kudhibiti uingizaji wa mifungo kutoka nje ndani ya bonde hilo.

Katika hatua nyingine, aliuagiza Uongozi wa Tawa kuhakikisha inakamilisha uwekazi wa mipaka ya hifadhi kwa kufikisha asilimia 50 ndani ya muda wa miezi mitatu kuanzia sasa kutoka iliyotelewa kwa kushirikiana na viongozi wa wilaya tatu za Kilombero, Ulanga na Malinyi pamoja na wananchi wa maeneo husika kwa kuwa kiwango kilichofanyika ni cha asilimia ndogo tofauti na muda uliotumika.

Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen Kebwe alisisitiza kuwa siku 14 alizozitoa kwa watu wote waliopo ndani ya ardhioefu ndani ya hifadhi ya bonde hilo, kuondoka mara moja na muda huo ikimalizika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Mratibu wa Uhifadhi wa Ardhioevu Bonde la Kilombero Kanda ya Mashariki, Pellage Kauzeni alisema kuwa asilimia kubwa ya wakazi wa vitongoji na vijiji mbalimbali, vilivyoanzishwa ndani ya hifadhi ya Bonde la Kilombero ni wavamizi, kwa vile hawana uthibitisho wowote wa barua kutoka serikali za vijiji