JPM aibua uozo mpya Bandarini

RAIS John Magufuli amesema amebaini madudu mengi yanayoendelea katika Bandari ya Dar es Salaam, ikiwemo kuwepo kwa makontena mengine yenye mabaki ya mchanga wenye madini ya dhahabu (makinikia).

Pia ametoa siku tano kwa Waziri wa Madini, Angela Kairuki na Waziri wa Kilimo na Chakula, Dk Charles Tizeba kusimamia utekelezaji wa majukumu yaliyo chini ya wizara zao, vinginevyo watalazimika kuachia nafasi zao. Aliyasema hayo Dar es Salaam jana baada ya kumwapisha Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko aliyemteua hivi karibuni kushika wadhifa huo na kufanya wizara hiyo kuwa na Naibu Waziri wawili.

Akizungumzia madudu bandarini, Rais Magufuli alisema alipotembelea bandari hiyo Septemba mwaka jana, aliunda timu ya siri ambayo ilihusisha wajumbe mbalimbali wakiwemo kutoka Jeshi la Ulinzi wa Wananchi (JWTZ), Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili kuichunguza kwa kina zaidi bandari hiyo.

“Yanayoendelea kugundulika ni maajabu, ukienda Ubungo pale mpaka kuna makontena ya makinikia, mpaka kuna vitu vingine vya ajabu vimekwisha ‘expire’ (kwisha muda wake wa matumizi), hiyo ndiyo Tanzania,” alisema Rais Magufuli. Aidha, alifichua kuwa kuna makontena zaidi ya 170, ambayo hayajulikani ni ya nani yakiwa bandarini pamoja na kwenye bandari kavu.

Rais Magufuli aliwataka viongozi wote kila, mmoja kughulikia eneo lake kwa hali ya juu na kwamba wasisubiri kuoneshwa uozo unaoendelea ndani ya taasisi walizopo. Alisema ni vema kama watendaji mbalimbali ambao mamlaka ya uteuzi yako kwake, kukataa uteuzi mara anapowateua kama watafahamu kuwa hawana uwezo wa kusimamia majukumu anayowapangia, hususani kuwatumikia wananchi wanyonge na si kukubali na baadaye kushindwa kufanya kazi husika.

Utendaji Wizara ya Madini Rais Magufuli alisema haridhishwi na utendaji kazi wa Wizara ya Madini na kwamba mambo mengi hayajafanyika mpaka sasa tangu kuundwa kwa wizara hiyo. Akiizungumzia Wizara ya Madini, Rais Magufuli alisema wizara hiyo inazo changamoto nyingi, ambazo mpaka sasa bado hazijapatiwa ufumbuzi pamoja na kuteuliwa kwa watendaji mbalimbali kwenda kuzishughulikia.

“Kila mtu anayepelekwa Wizara ya Madini inakuwa kuna kama pepo fulani linawabadilisha akili, maana ni kweli pale kuna hela na dhahabu zinawazunguka na haya ni mapepo. “Kwa hiyo yanawabadilisha akili, mnateuliwa mkiwa na akili zenu lakini mkiingia pale mnabadilika hamchukui hatua nzuri, mkigeuka huku dhahabu, huku almasi, huku Tanzanite. Sasa muende mkashindane nayo kwa kumtanguliza Mungu,” alisema Rais Magufuli.

Alisema Julai mwaka jana, Bunge lilipitisha Sheria ya Madini Namba 7 ya Mwaka 2017 baada ya kufanyiwa marekebisho sheria iliyokuwepo, lakini mpaka sasa wizara hiyo haijatengeneza Kanuni zake. Rais Magufuli alitoa maelekezo kuwa kabla ya Januari 12, mwaka huu Kanuni za Sheria hiyo ya Madini ziwe zimesainiwa ili ziweze kuanza kufanya kazi.

“Sasa Wizara ina Naibu Waziri wawili na Waziri mmoja, nitashangaa sana kama Kanuni hizo hazitasainiwa, nataka kabla ya Ijumaa wiki hii kanuni hizi ziwe zimeshasainiwa. “Nilitoa maelekezo watendaji washughulikie Kanuni lakini mpaka sasa hazijasainiwa, Waziri yupo, Naibu wake yupo, Makatibu wakuu wapo, Kamishna wa Madini ambaye ndio Mshauri Mkuu wa Waziri yupo.

Unaweza kuona tuna matatizo makubwa kiasi gani serikalini,” alisema Rais Magufuli. Alisema baada ya kutungwa sheria hiyo mpya, Watanzania waliamini mambo mengi ya madini yatanyooka ndiyo maana yeye aliisaini siku hiyo hiyo, jambo ambalo halikuwa hivyo, alisema sasa ameamua kuongeza Naibu Waziri mwingine katika wizara hiyo ili kuongeza nguvu.

“Najua Waziri wa Madini yuko likizo, sifahamu sheria zinazungumzaje, kama Naibu Waziri haruhusiwi kusaini kanuni hizo basi Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Kabudi (Palamagamba) asaini, mkakae mpitie,” alisema.

Rais Magufuli alisema kama hazitatengenezwa Kanuni hizo, mtu ambaye atavunja sheria katika sekta hiyo, haitawezekana kumpeleka Mahakamani. “Baadhi ya ninaowateua hawajaelewa nataka nini, Bunge linataka nini na Watanzania wanataka nini, sioni ‘movement’ ninayoitaka. Sijui Wizara hii ina matatizo gani,” alisisitiza Rais Magufuli.

Alisema kwa kumteua Naibu Waziri huyo, ambaye alikuwa kwenye Kamati ya Bunge ya Kuchunguza Madini, itasaidia kutoa ushauri na mapendekezo ambayo yalikuwa yakitolewa bungeni ili kutoa changamoto ya kuwaamsha watendaji katika wizara hiyo ambao alisema bado wamelala. Rais Magufuli alisema serikali itashindwa kukusanya mapato stahiki kwa kupitia sheria hiyo, kama hakutakuwa na Kanuni, ambapo alitoa maelekezo kwamba usifanyike mnada wowote wa madini mpaka Kanuni zisainiwe.

Alisema kuna viongozi ambao wana hisa kwenye kampuni za kuchimba madini na wengine wanashirikiana na ndugu zao au kuandika kampuni zao majina ya ndugu. “Kabudi nakupa kabla ya Ijumaa kakae na Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu na Wakurugenzi. Waziri nimempa likizo, ziwe zimesainiwa na ziwe zimeanza kazi. Inawezekana maneno yangu haya hayawafurahishi baadhi ya wanasiasa, mimi si mwanasiasa,” alisema.

Alimpongeza Naibu Waziri wa Wizara ya Madini, Stanslaus Nyongo ambaye amezungukia migodi ya madini, hata hivyo ametoa maelekezo kuwa washughulikie wizara hiyo nzima. Amtumbua Kamishna wa Madini Pamoja na maagizo hayo, Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Kamishna wa Madini, Benjamin Mchwampaka na amemteua Profesa Shukrani Elisha Manya kuwa Kamishna wa Madini na pia kukaimu nafasi ya Mtendaji Mkuu wa Kamisheni ya Madini.

Kabla ya uteuzi huo, Profesa Manya alikuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Idara ya Jiolojia. Rais Magufuli alisema ameamua kutengua uteuzi wa Mchwampaka, kutokana na malalamiko kuwa amekuwa ni kikwazo katika wizara hiyo.

“Kamishna anawapendelea wale badala ya kupendelea serikali, haya ni maajabu makubwa… Nililetewa mapendekezo ya watu wa palepale (wizarani) lakini nikasema nisichukue kabisa watu wa hapo, nipate mtu ambaye hajawa ‘contaminated’, ndiye atakuwa Kamishna na Mtendaji Mkuu wa taasisi ili mambo yaanze, hadi nitakapoamua vinginevyo,” alisema Rais Magufuli.

Aliwataka pia makatibu wakuu katika wizara ya madini kuwa wakali kwa watendaji, ikiwezekana kuwaondoa watu ambao watafanya kazi. Dk Tizeba naye mtegoni Kuhusu Wizara ya Kilimo na Chakula, Rais Magufuli ameiagiza wizara hiyo kuhakikisha inasimamia ili mbolea iweze kuwafikia wakulima katika mikoa inayotegemewa kwa kilimo, ukiwemo Mkoa wa Rukwa ifikapo Januari 12, mwaka huu. Aidha, amemwelekeza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufuatilia jambo hilo na endapo mbolea haitafikishwa katika maeneo hayo ifikapo siku hiyo, wahusika waache kazi wenyewe.

“Wakulima wanataka mbolea na muda ni huu, inasikitisha sana, lakini ninapozungumza hapa ipo mikoa kama Rukwa na mingine ambayo haijapelekewa mbolea, na kwenye bajeti Waziri alipitisha,” alisema. Rais Magufuli aliwataka watendaji wote wa Serikali, kutekeleza majukumu yao ipasavyo. Alionya kuwa hatasita kumfukuza kazi mtendaji yeyote, atayeshindwa kutekeleza wajibu wake kwa maslahi ya Watanzania.

Aidha, alisema sekta mbalimbali zikisimamiwa vizuri, nchi itaondokana na umasikini. Aliwataka pia kila mtendaji kwa nafasi yake kuchukua majukumu yake katika kutatua changamoto za Watanzania. Amuapisha Biteko kuwa Naibu Waziri Awali Rais Magufuli alimuapisha Biteko ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe, na kumpa maelekezo ya kwenda kushughulika na wizara hiyo ambayo mpaka sasa kasi yake haijamridhisha.

Rais Magufuli alisema anampongeza Biteko kwa kupata nafasi hiyo ya uongozi, lakini anampa pia pole, kwani kufukuzwa ni kitu cha kawaida, kama hatakwenda kutenda kazi aliyopewa. “Nakupongeza Biteko lakini nakupa pole, sikufichi kwa sababu kwangu kufukuzwa ni kitu cha kawaida, ukafanye kazi, na mkifanya kazi nitawapongeza kwa sababu ndiyo jukumu letu la kuwatumikia Watanzania,” alisema.

Rais Magufuli alisema Serikali imeamua kuanzisha Kampuni ya Serikali ili kuhakikisha inalinda madini pamoja na mapato yake. Aidha, Rais Magufuli aliwataka viongozi kuwa mfano bora na pia kuchapa kazi ambayo italeta manufaa kwa Watanzania wote. “Kazi hizi ndugu zangu ni mateso na ni msalaba mkubwa, haya mambo tunayoyafanya msifikiri watu wote wanafurahi, inawezekana kuna mataifa makubwa yanachukia kwa nini Tanzania mnafanya miradi mikubwa ya maendeleo peke yenu.

“Hii ni vita na kuna maadui wengine wanajulikana na wengine hawatajulikana, lakini kama taifa ni lazima kusimama imara na kuweka nguvu katika kusaidia wananchi. “Kazi hizi si nyepesi, ni lazima kujikana na kujitoa kwa ajili ya watu, kila kiongozi niliyemchagua ni lazima afuate hilo amtangulize Mungu wake na ajitoe kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi ambao ni wanyonge,” alisema Rais Magufuli. Alilipongeza pia Bunge pamoja na Spika wake, Job Ndugai kwa mhimili huo kuwa na msaada na manufaa makubwa katika kutatua changamoto za wananchi.