Lowassa: Rais umenipa faraja

RAIS John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo hayo, Lowassa amempongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya na kuongeza kuwa amepata faraja kufika Ikulu kuonana na Rais. Taarifa iliyotolewa na Ikulu kwa vyombo vya habari, ilisema Lowassa ambaye alikuwa mgombea urais kupitia Chadema katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, na ambaye kwa sasa ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alifika Ikulu jana.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baada ya mazungumzo, Lowassa alimpongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya na alitaja baadhi ya maeneo ambayo kazi kubwa imefanyika kuwa ni kutoa elimu bila malipo. Miradi mingine ni ujenzi wa mradi wa uzalishaji wa umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge), ujenzi wa viwanda na ujenzi wa reli kwa kiwango cha kisasa (standard gauge), ambavyo vinazalisha ajira nyingi kwa Watanzania.

“Nimepata faraja sana kuja hapa Ikulu kuonana na Rais, tumezungumza naye na nimempongeza kwa kazi nzuri anayoifanya, lazima tukiri anafanya kazi nzuri na anahitaji kutiwa moyo. “Moja kubwa ambalo ni la msingi sana ni la kujenga ajira, katika kuanza ujenzi wa reli ya kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro hapo anajenga ajira, na kwenye nchi yoyote inayoendelea suala muhimu ni kujenga ajira.

“Stieglers Gorge ni kujenga ajira na mingine ya aina hiyo, lazima kuwepo na kipaumbele cha kusema kwamba tunajenga ajira, jingine ni la elimu, ni muhimu sana, hauwezi kuacha elimu katika mambo yako unayofanya, hili nalo lazima lisemwe vya kutosha, kwa kweli nakushukuru Rais, you made my day,” alisema Lowassa.

Kwa upande wake, Rais Magufuli alimpongeza Lowassa kwa kutambua kazi kubwa, inayofanywa na serikali na alisema ni mmoja wa viongozi ambaye kwa wakati wake, ametoa mchango wake katika nchi. Rais Magufuli aliongeza kuwa Lowassa ni mwanasiasa mzuri, kwani hata wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita, ambao naye aligombea kiti cha Urais, hakuwahi kumtukana.

“Lowassa ameniomba mara nyingi nikutane naye, na leo nimekutana naye, tumezungumza mambo mengi, ameniambia ya kwake na mimi nimemwambia ya kwangu. “Kwa ujumla Lowassa ni mwanasiasa mzuri na tuendelee kuwaenzi wazee hawa ambao kwa nyakati fulani walifanya mambo mazuri, na mimi napenda kumpongeza Lowassa ambaye kama alivyosema hapa kuwa tumefanya mambo mazuri mengi.

“Ametaja miradi mbalimbali tunayotekeleza, ametaja mradi wa Stiegler’s Gorge utakaogharimu zaidi ya Shilingi trilioni 7, amezungumzia juu ya elimu bure, amezungumzia juu ya maji ambayo kwa bahati nzuri yeye alikuwa Waziri wa Maji na anafahamu sasa tumefikia wapi, amezungumza juu ya umeme tulivyosambaza katika vijiji mbalimbali, elimu bure, huduma za hospitali na mengine,” alisema Rais Magufuli.