Waliojenga mapitio ya maji dar kubomolewa

MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi amesema wananchi waliojenga nyumba na kuta katika maeneo yaliyokuwa mapitio ya maji, wabomoe nyumba zao kabla manispaa haijabeba jukumu hilo litakalowagharimu.

Amesema wananchi watakaokaidi kufanya hivyo kwa muda watakaopewa, watabomolewa nyumba zao na manispaa hiyo na kwamba, watu hao watatakiwa kuilipa fidia na gharama za ubomoaji.

Naye Msimamizi wa Mradi wa Uboreshaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP), Mkelewe Kungalaza, alisema watatoa notisi ya siku saba kwa wananchi wote waliojenga kwenye maeneo yanayopita maji ili kuvunja nyumba zao na kwamba wasipofanya hivyo, watawavunjia na kuwapeleka mahakamani ili walipe fidia.

Akizungumza katika ziara ya kutembelea barabara zilizojengwa na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura), Mkuu wa Wilaya alisema serikali imegharamia zaidi ya Sh bilioni 23.1 kwa ajili ya kujenga miundombinu ya barabara.

Hapi alisema ni jambo la ajabu kuona mtu anajenga ukuta au nyumba ya ghorofa katika eneo linapopitisha maji hali aliyosema inasababisha kuyazuia na hivyo, kuchangia kuleta maafa ya mafuriko wakati wa mvua.

‘’Wakati mwingine serikali inalaumiwa kutokana na mafuriko ya maji kuleta maafa kwa wakazi wetu, lakini chanzo kikubwa ni uharibifu unaofanywa na wananchi katika maeneo ambayo maji yamejiwekea njia yake hivyo kusababisha maji kukosa njia na kuingia kwenye makazi ya watu,’’ alifafanua Hapi.