Elimu yarejesha wasiofikia wastani shule walizotoka

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeziagiza shule zote zilizokaririsha, kuhamisha na kuwafukuza shule wanafunzi kwa kigezo cha kutofi kia wastani wa ufaulu wa shule, kuwarejesha shuleni wanafunzi hao ifi kapo Januari 20, mwaka huu ili waendelee na masomo yao katika madarasa ambayo wanapaswa kuwepo kisheria.

Mbali na kuwarejesha shuleni, wametakiwa kuhakikisha wanafunzi hao wanaandikishwa kufanya mitihani yao ya mwisho katika shule hizo na siyo vituo tofauti. Aidha, wazazi na walezi wa wanafunzi ambao watoto wao walirudishwa nyumbani wanapaswa kuwapeleka shuleni wanafunzi hao katika muda uliotajwa na wizara ili wanafunzi hao waendelee na masomo.

Hayo yamebainishwa na Kamishna wa Elimu nchini, Dk Edicome Shirima katika taarifa yake kwa umma aliyotoa jana. Katika taarifa hiyo, Dk Shirima alisema Waraka wa Elimu Namba 7 wa Mwaka 2004 umepiga marufuku utaratibu wa shule zisizo za serikali kukaririsha darasa au kuhamisha mwanafunzi aliyefanya na kufaulu mtihani wa darasa la nne, kidato cha pili na cha nne kwa kigezo cha wanafunzi hao kutofikisha wastani wa ufaulu wa shule husika.

Alisema waraka huo umeeleza wazi kuwa ni marufuku kufanya vitendo hivyo vya kinyanyasaji kwa wanafunzi, wazazi na walezi na kwamba shule yeyote itakayobainika kukiuka taratibu za wizara itachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kutoruhusiwa kusajili wanafunzi.

Aliongeza pamoja na kutolewa kwa waraka huo, hivi karibuni wizara imebaini kuwepo kwa baadhi ya shule zisizo za serikali kuharirisha na kuhamisha wanafunzi kwa kigezo cha kutofikia wastani wa ufaulu wa shule.

“Baadhi ya wakuu wa shule wamefikia hatua ya kuwatuhumu wanafunzi kuwa na makosa ya utovu wa nidhamu na kisha kuwaeleza wazazi na walezi wa wanafunzi husika kuwa adhabu ni kurudia darasa au kuwarejesha shuleni kwa masharti ya kuwatafutia shule au vituo vingine vya kufanyia mitihani yao ya mwisho, jambo ambalo ni kinyume na taratibu na sheria, miongozo na taratibu zilizowekwa na wizara,” alisema Dk Shirima.

“Kutokana na ukiukwaji huo wa taratibu zilizowekwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuanzia leo tarehe 12 Januari, 2018 wizara inaziagiza shule zote zilizokaririsha, kuhamisha au kufukuza shule wanafunzi kwa kigezo cha kutofikia wastani wa ufaulu wa shule kuwarejesha wanafunzi hao ifikapo tarehe 20/1/2018 ili waendelee na masomo katika madarasa ambayo wanapaswa kuwepo kisheria na wahakikishe kuwa waandikishwa kufanyia mitihani yao ya mwisho katika shule hizo na siyo vituo tofauti,” alibainisha Kamishna wa Elimu.

Aidha, alisema shule ambayo itakaidi agizo hilo, wizara itawachukulia hatua za kisheria ikiwemo kuwafungia usajili wa wanafunzi na kufutiwa usajili wa shule, pia wizara inawakumbusha wamiliki na waendeshaji wote wa shule kuzingatia sheria, miongozo na taratibu zilizowekwa na wizara.