Mvua yaua, vijiji vyazingirwa na maji

WATU wawili wamefariki dunia, mmoja kwa kusombwa na maji ya mafuriko ya mvua katika Mto Mkondoa wilayani Kilosa na mwingine kuangukiwa na mti kwenye nyumba yake akiwa ndani katika Manispaa ya Morogoro.

Watu hao majina yao hayakuweza kupatikana mara moja, walifariki juzi kwa nyakati tofauti, ambako aliyefariki Kilosa alikuwa akivuka mto uliojaa maji ya mvua zilizonyesha juzi na kusababisha Mto Mkondoa kufurika maji.

Mkuu wa Mkoa huo, Dk Stephen Kebwe alithibitisha jana kutokea kwa vifo hivyo vilivyosababishwa na mvua kubwa zilizokuwa zimenyesha katika baadhi ya wilaya za mkoa huo.

Alisema aliyefariki katika Manispaa ya Morogoro ni mwanamke mwenye kukadiriwa kufikia umri wa miaka 50 ambaye aliangukiwa na mti kwenye nyumba yake iliyopo Mtaa wa Forkland alipokuwa ndani kutokana na upepo mkali ulioambatana na mvua.

Dk Kebwe alisema kwamba kamati za maafa za wilaya za mkoa huo zitafanya tathmini ya awali ya kujua madhara yaliyojitokeza ili hatua mbalimbali zichukuliwe. Mvua zilizonyesha juzi katika baadhi ya wilaya pamoja na Manispaa ya Morogoro zilisababisha baadhi ya mitaa kujaa maji kutokana na mitaro kujaa uchafu uliokuwa umesombwa na maji hayo na baadhi ya nyumba kujaa maji na kuzingirwa.

Aidha, jana jioni imebainika kuwa vijiji vitatu vya Malui, Tindiga na Kimamba A katika Wilaya ya Kilosa vimezingirwa na maji ya mvua kubwa zilizonyesha juzi na Mto Mkondoa umefurika na kutishia usalama wa tuta lililojengwa kuzuia maji kuingia katika makazi ya watu mjini Kilosa.

Mkuu wa mkoa, Dk Kebwe alitarajiwa kuzuru vijiji hivyo kujionea athari ya mvua hizo ambazo juzi mkoani Dodoma, zilisababisha usafiri wa Kanda ya Kati na nchi jirani kuvurugika kutokana na magari zaidi ya 600 kukwama eneo la Mtanana katika mji wa Kibaigwa wilayani Kongwa, kujaa maji.