Serikali yatoa bilioni 25/- kujenga, kukarabati meli

SERIKALI imetoa Sh bilioni 24.5 kujenga meli mpya mbili na kukarabati meli tano ili ziweze kutoa huduma ya uchukuzi wa kusafi risha abiria na mizigo katika maziwa makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.

Hayo yalielezwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano jana, Atashasta Nditiye wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu ujenzi wa meli katika Maziwa Makuu kwenye kikao kilichofanyika bungeni mjini Dodoma.

Nditiye alisema kuwa fedha hizo tayari zimeshatolewa naSerikali na kupatiwa kampuni ya MSCL kwa ajili ya kuanza ujenzi wa meli 2 mpya za kubeba abiria na mizigo katika ziwa Tanganyika na Victoria na kukarabati meli 5 ambazo ni Mv Victoria, Mv Butiama, Mv Liemba, Mv Umoja na Mv Serengeti.

Nditiye (pichani) alisema kuwa lengo la Serikali la kutoa fedha hizo ni kuboresha huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo katika maziwa makuu ili wananchi waweze kupata huduma za usafiri wa uhakika.

Pia alisema kuwa uwepo wa huduma hizo utasaidia wananchi kutambua fursa ya biashara iliyopo kwenye maziwa hayo kwa kuzingatia kuwa meli hizo ni kiungo kikubwa baina ya nchi yetu na nchi za jirani za Uganda, Kenya, Zambia, Malawi na DRC Congo kwa kuwa zinatumia meli zetu kusafirisha abiria na mizigo yao kupitia maziwa hayo.

Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya MSCL, Eric Hamissi alisema kuwa tayari kampuni yake kwa kushirikiana na wataalamu wa kampuni hiyo na wengine kutoka wizara yenye mamlaka, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) na Jeshi la Ulinzi la Wananchi, Kitengo cha Wanamaji wamekamilisha taratibu za kumpata mkandarasi wa kujenga meli mpya ya Ziwa Victoria.

Mkandarasi aliyepewa kazi hiyo ni Kampuni ya STX Engine Co. Ltd na STX Offshore & Shipbuilding Co. Ltd Joint Venture; na mkandarasi wa Kampuni ya KTMI kwa kushirikiana na Kampuni ya Yuko’s Enterprises Co. Ltd kwa ajili ya kukabarati meli za Mv Victoria na Butiama. Meneja huyo alisema kuwa kampuni hizo zimekidhi vigezo vya mahitaji ya meli ya kubeba abiria na mizigo na zina teknolojia ya kisasa ya ujenzi na ukarabati wa meli ili kufikia azma ya Serikali ya kutoa huduma nzuri kwa abiria na wananchi wake.

Akizungumzia meli zilizokarabatiwa hivi karibuni kwa Sh milioni 300 kutoka TPA, Hamissi alisema kuwa mamlaka hiyo ya bandari ilikarabati meli nne za Kampuni ya MSCL za kubeba mizigo na abiria ambazo ni Mt Sangara, Mv Clarias, Ml Wimbi na Mv Umoja ambazo zimeanza kazi.

Alisema zitaiwezesha kampuni ya MSCL kujiendesha, kufanya kibiashara na kuongeza mapato ya Serikali kwa kutoa huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo kwenye mwambao wa maziwa makuu na nchi za jirani.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Profesa Norman Sigalla aliiipongeza Serikali kwa kutoa fedha za kujenga na kukarabati meli za maziwa makuu ya Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa.

Aidha, Prof Sigalla aliishaurii Serikali iajiri wafanyakazi wa meli wenye vigezo vya kimataifa kwa kuwa wengi waliopo wanakaribia kustaafu na ameitaka MSCL kutumia fedha hizo kama zilivyopangwa na kwa wakati ili wananchi wapate huduma za usafiri bora zaidi kwenye maziwa makuu. Hata hivyo, Naibu Waziri alisema serikali inakabiliana na changamoto ya upungufu wa manahodha wa meli kwa kuzalisha wataalamu hao wenye weledi wa kisasa kutoka kwenye Chuo cha Bahari cha Dar es Salaam (DMI) na Jeshi la Ulinzi la Wananchi, Kitengo cha Wanamaji.