Mafuriko ya Kibaigwa yatia hofu wabunge

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeonesha hofu kwa viongozi wakuu wa kitaifa wanaofanya safari kuelekea Makao Makuu ya nchi Dodoma, kudhurika kutokana na maji ya mvua kufunika barabara mara kwa mara katika eneo la Kibaigwa.

Kutokana na kutanda kwa hofu hiyo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amekubali ombi la wajumbe wa Kamati hiyo la kuambatana nao ili kufika katika eneo hilo ili kukagua na kubaini kiini cha hali hiyo. Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge, Profesa Norman Sigala wakati kamati hiyo ilipokutana na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) katika ukumbi wa Bunge mjini hapa jana.

“Kamati imeona eneo lile ni hatari sana. Viongozi wetu wakuu wanasafiri sana kwa barabara hivi sasa kuja yalipo Makao Makuu Dodoma. Hatuwezi kukubali kuona viongozi wanapita katika maeneo hatarishi kama haya. “Dereva anaweza kuingiza tairi halafu ghafla akasababisha madhara kwa kiongozi. Lakini si viongozi tu hata wananchi pia wanaosafiri katika barabara hii ya Dodoma- Morogoro na kupita eneo hilo wakati wa mvua maisha yao yanakuwa hatarini.

“Hebu jaribu kufikiri wakati wa usiku, maji ya mvua yanaweza kuwa yanakuja kwa kasi madereva wasijue na hatimaye magari yanaweza kusombwa na kusababisha madhara makubwa kwa abiria na mali zao,” alisema Profesa Sigala.

Alisema mbali ya barabara hiyo ya Dodoma- Morogoro, ambayo hivi karibuni ilisababisha magari yanayokwenda na kutoka Mikoa ya Kanda ya Kati na nchi jirani kushindwa kupita katika eneo hilo kwa saa nane, Kamati hiyo imeagiza pia barabara ya Dodoma- Iringa katika eneo la Fufu kutazamwa. “Hili nalo ni eneo hatari sana kwa viongozi na wananchi wanaosafiri kuja Makao Makuu ya nchi kwani maji hujaa na kufunga barabara kwa muda mrefu mara kwa mara.