Magufuli asitisha usajili meli mpya

RAIS John Magufuli amewaagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasliano, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafi rishaji wa Zanzibar, Balozi Ali Abeid Karume, kusitisha usajili wa meli mpya hapa nchini mpaka hapo itakapotangazwa vinginevyo.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo jana, alipozungumza na wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, kikao ambacho kimehudhuriwa na mawaziri hao.

Alitoa agizo hilo ili kujipanga upya kutokana na taarifa za kukamatwa kwa dawa za kulevya katika meli zinazopeperusha bendera ya Tanzania, ambazo hadi sasa zimefi kia meli tano.

Mbali na kusitishwa kwa usajili mpya wa meli, Rais Magufuli aliwaagiza mawaziri hao pamoja na vyombo vya dola, kufanya uchunguzi wa kina kwa meli zote 470 zilizosajiliwa nchini na zinapeperusha bendera ya Tanzania.

Aidha, Rais Magufuli alimuagiza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga kusimamia utekelezaji wa maagizo hayo na kuhakikisha jina la Tanzania halichafuliwi ndani na nje na nchi.

“Kafanyeni uchunguzi wa kina kwa meli zote zinazopeperusha bendera ya Tanzania, fanyeni uchunguzi kwa meli zilizokamatwa ambazo ni 5 na pia hizi 470 zilizosajiliwa na zinazoendelea kufanya kazi zichunguzeni, hatuwezi kuacha jina la nchi yetu lichafuliwe na watu wanaofanya mambo kwa maslahi yao,” alisema Rais Magufuli.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Rais Magufuli alitaka maagizo yote yaliyotolewa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kuhusu meli hizo yatekelezwe. Juzi, Makamu wa Rais alitangaza kuwa serikali imezifutia usajili meli mbili zilizokamatwa kwa kupakia shehena za dawa za kulevya na silaha kinyume cha sheria, huku zikiwa zinapeperusha bendera ya Tanzania.

Aidha, alisema itaanzisha utaratibu wa kuzifanyia uchunguzi wa kina meli zote mpya, zitakazoomba usajili pamoja na wamiliki wake kwa kushirikisha vyombo mbalimbali vya serikali, vikiwemo vile vya ulinzi na usalama ili kuondokana na utata na dosari zinazoharibu sifa njema ya nchi.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amewataka wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kutilia mkazo utekelezaji wa sera ya diplomasia ya uchumi ili nchi inufaike na fursa mbalimbali za uhusiano na ushirikiano na mataifa mengine duniani.

Rais Magufuli alimuagiza Balozi Mahiga kuhakikisha Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi, na wakurugenzi wa idara za wizara hiyo, wanafanya kazi zenye manufaa kwa nchi, ikiwemo kuwataka mabalozi kutoa taarifa kila baada ya robo mwaka juu ya ukusanyaji wa mapato na utekelezaji wa sera hiyo.

“Wakupe taarifa kila baada ya robo mwaka, na balozi ambaye atakuwa hakusanyi mapato vizuri na kuinua biashara na uwekezaji atakuwa hafai kuendelea kuwa balozi, tena kawaambie kabisa kwenye suala hili hakuna mchezo,” alisisitiza Rais Magufuli