Sugu kuendelea kusota rumande

MATUMAINI ya mashabiki wa Chadema waliojazana mahakamani jana, wakiamini mbunge wao, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu, atapewa dhamana katika kesi inayomkabili ya kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli, yaliingia shubiri baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi kuzuia dhamana hiyo.

Uamuzi huo ulifikiwa na Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya, Michael Mteitei aliyesema mahakama imepanga kusikiliza kesi hiyo kwa muda mfupi kama nyingine na kutoa uamuzi ndani ya wiki moja.

Alisema kabla ya kufikia uamuzi, mahakama ilijiuliza, je ikitoa dhamana kwa washitakiwa, je wataweza kuhudhuria mahakamani kwa muda na siku iliyopangwa na kuona kuwa ikitoa dhamana kesi haitosikilizwa kwa muda mfupi kama ilivyopanga.

Mteite alisema mahakama imeamua washitakiwa wote wawili, wataendelea kukaa mahabusu hadi Januari 22, mwaka huu ambako upande wa mashitaka utasoma uchambuzi wa awali wa kesi hiyo na kwamba siku inayofuata Januari 23, itakuwa ni zamu ya upande wa utetezi.

Baada ya kusoma uamuzi wa mahakama, wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliokuwa wamejazana ndani ya ukumbi wa mahakama, baadhi yao walikwenda na kusimama nje ya geti la kutokea gari mahabusu wakipiga kelele kushinikiza Sugu apewe dhamana.

Mashabiki hao wa Chadema walidai kuwa dhamana ni haki ya mshitakiwa na kwamba kwa mujibu wa Katiba, kosa lake linadhaminika hivyo ni lazima mahakama itoe dhamana ama la wawakamate wote waende gerezani.

Kutokana na sintofahamu hiyo, polisi walilazimika kuongeza ulinzi, huku gari la polisi maarufu kama karandinga lililombeba mbunge huyo na watuhumiwa wengine, liliondoka mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali wa polisi waliokuwa kwenye msafara wa magari manne.

Mbilinyi pamoja na mshitakiwa mwenzake, Katibu wa Chadema Kanda, Emmanuel Masonga walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Januari 16, mwaka huu, wakishitakiwa kwa kosa moja la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais Magufuli.

Washitakiwa wote walipelekwa mahabusu baada ya Wakili wa Serikali, Joseph Pande kupinga dhamana kwa washitakiwa kwa ajili ya usalama wao, wakati wakili wa utetezi akipinga hoja hiyo na kuilazimu Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya kuamuru mbunge huyo kupelekwa mahabusu.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali, Pande kuwa watuhumiwa wote wawili wanashitakiwa kwa shitaka moja la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais Magufuli kinyume cha sheria.