Vijana wahimizwa kilimo cha kibiashara

VIJANA wameshauriwa kujikita kwenye kilimo cha biashara kwa sababu ndiyo sekta inayoweza kuwaajiri wengi zaidi na vizuri, tofauti na nyingine.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Amsha Institute of Rural Enterprenuership, Omary Mwaimu alisema hayo jana katika Jukwaa la Tatu la Ujasiriamali lililofanyika Chuo Cha Usimamizi wa Fedha (IFM), jijini Dar es Salaam.

Mwaimu ambaye pia ni mkulima alisema kilimo ni zaidi ya kuchimba na kufukia mbegu kwa ajili ya mazao ya chakula, bali ni biashara kinapoendeshwa kitaalamu na kuenziwa.

Mwakilishi kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Gili Tery alisema wanawaelekeza vijana kuhusu vitu vitakavyowasaidia kupata fursa ya kujitengenezea ajira ikiwa ni pamoja na fursa zilizopo na masoko yaliyopo ndani na nje ya Tanzania, na namna ya kuanza taratibu za kuanzisha biashara na kujisajili.

Mkuu wa Kitivo cha Uchumi na Sayansi ya Uongozi chuoni hapo IFM, Dk Godwin Kaganda alisema, mada ya jukwaa hilo ni ‘Maendeleo Tanzania, fursa na changamoto kuelekea Tanzania ya Viwanda’.