Zuma apewa saa 48 kujiuzulu

 Chama tawala nchini Afrika Kusini, ANC kimekubali kumuondoa rais Jacob Zuma kama kiongozi wa taifa hilo, vyombo mbalimbali vya habari vya nchini Afrika Kusini vimeripoti.

Hatua hiyo inafuatia kikao kilichochukua saa 13, kilichojumuisha maofisa wa juu wa chama. Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ujerumani (DW), katibu mkuu wa ANC amekwenda kuonana na Rais Jacob Zuma ili kumuarifu kuhusu uamuzi huo wa chama wa kumwondoa madarakani.

Taarifa za mapema leo kutoka ndani ya Kamati Kuu ya chama hicho yenye wajumbe 107, iliyokutana kuanzia siku jana na leo kujadili kuhusu mustakabali wa Zuma, zimesema Zuma amepewa saa 48 ya kujiuzulu, baada ya wiki moja ya minong’ono kuhusu hatma ya kiongozi huyo.

Miongoni mwa vyombo vilivyoripoti taarifa hii ni pamoja na Shirika la Habari la Serikali (SABC) ambalo limearifu kwamba ANC imempa Rais Zuma saa 48 za kuachia madaraka. Hata hivyo hakujatolewa taarifa rasmi na maafisa wa ANC hawakupatikana kuthibitisha taarifa hiyo.

Taarifa zaidi zinasema Chama cha ANC kitafanya mkutano na waandashi wa habari majira ya saa nane mchana leo kuzungumzia matokeo ya kikao hicho na mustakabali wa Rais Jacob Zuma.

Kabla ya kikao cha Kamati Kuu kumalizika, Makamu wa Rais, Cyril Ramaphosa aliripotiwa kuondoka kwenye kikao hicho ambacho kiliendelea hadi usiku wa manane, ili kukutana na Zuma kwenye makazi yake rasmi yaliyoko Pretoria.

Msafara wake ulionekana kurejea kwenye ukumbi kulipokuwa kunafanyika kikao hicho usiku wa manane, na saa tatu baada ya kurejea kikao hicho kikafungwa. Rais Jacob Zuma (75) aliingia madarakani Mei 2009, akichukua nafasi ya mtangulizi wake, Thabo Mbeki.