TUCTA yaomba huruma ya serikali vyeti feki

SERIKALI imepokea maombi ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), wakiomba huruma ya serikali kwa watumishi ambao walikutwa na vyeti feki ili wapatiwe mafao yao kwa wengine waliitumikia serikali kwa muda mrefu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipotembelea Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na kuzungumza na watumishi wake.

“Serikali ilishatoa ufafanuzi tangu mwanzo kwamba, wale wote waliokutwa na vyeti feki, wana makosa, na mtu ukishapatikana na makosa; moja anaweza kushitakiwa kwa mujibu wa kanuni za serikali na kosa la pili anaweza kushitakiwa Takukuru(Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa), lakini serikali imetoa msamaha kwamba hakuna atakayeshitakiwa,” alisema na kuongeza:

“Sasa inakuja hoja, je! wanastahili kupewa mafao? Ukifanya uchambuzi wa mkataba wa kazi kati ya mwajiri na muajiriwa unasema, ili tukuajiri lazima ulete cheti chako na umepeleka cheti ambacho baadaye kimegundulika ni feki, je! huo mkataba ni halali au si halali?...

Ina maana mkataba huo ni feki sasa unapaswa kulipwa mafao kwa mkataba feki?”. Alisema, mpaka sasa serikali haijafanya uamuzi juu ya maombi hayo na tayari wameshafanya kikao na TUCTA na wameomba huruma ya serikali kwa kuwa wahusika wanamakosa kisheria.

“Serikali imeyapokea maombi hayo na tunayafanyia kazi na muda ukifika tutatangaza, ndiyo maana tunasema wameomba huruma kwa kuwa wanajua wahusika walikuwa wanatumikia mkataba feki, hivyo hakuna cha kulipwa,” alisema.

Alisema zipo hoja kwamba “Pamoja na cheti feki, mimi nimefanya kazi serikalini kwa muda mrefu, sasa naomba mnihurumie, ila ukidai kwa mujibu wa sharia, hakuna kitu hapo ndiyo mana tunasema TUCTA wameomba huruma ya serikali na inafanyia kazi maombi hayo, bado haijatoa uamuzi na uamuzi ukitoka tutawaambia”.

Akizungumzia hoja ya baadhi ya watumishi wanaodai serikali majina yao kutoonekana katika orodha alisema, uhakiki maana yake ni kuleta madai yote na uthibitisho kwamba unaidai serikali na baada ya hapo wanakaa watu wanayapitia, hivyo mtu akiwa haonekani kwenye orodha ana matatizo.

“Kama madai yako ni halali, kwa mfano kama ulipewa uhamisho na barua unazo unawasilisha…serikali inafanya kazi kwa maandishi, ukionesha unalipwa ila kama unaenda kudai kwa mdomo hakuna mtu atakulipa ila kama kuna mtu ana madai yake kwenye makaratasi yatafanyiwa kazi,” alisema.