Fursa lukuki reli ya kisasa

UJENZI wa tuta la Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, umewezesha Watanzania 1,413 na 1,162 wa kigeni kuajiriwa kwenye mradi huo katika fani mbalimbali.

Mradi huo ambao umefikia asilimia 20 tangu kazi ya ujenzi ianze mwezi Mei mwaka jana karibu miezi minane, sawa na siku 240, unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2019. Meneja wa Mradi huo kutoka Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahco), Maizo Mgedzi, aliliambia HabariLeo kuwa kazi ya ujenzi inaendelea vizuri. Alisema, Mkandarasi ameshasafisha asilimia 60 ya eneo ambalo reli itapita ambalo ni sawa na kilomita 120. Kazi hiyo ya ujenzi wa tuta la reli inajumuisha kazi ya kukata vilima na kujaza tuta.

Alisema, shughuli hiyo ya kusafisha eneo la ujenzi inahusisha kuondoa miti pamoja na majani. “Kazi za baadaye kwa mujibu wa mpangilio wa kazi, zitakuwa kutandika reli, kujenga madaraja, kujenga mifumo ya umeme, kujenga mifumo ya mawasiliano ya kuendeshea treni, kujenga majengo ya stesheni pamoja na kujenga karakana za kuhudumia usafiri wa treni,” alieleza Mgedzi.

Ikumbukwe kwamba, reli hiyo ya kisasa yenye urefu wa kilomita 205, ikijumuisha na kilomita 95 za njia ya kupishanisha treni na hivyo kufanya reli yote kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kuwa na jumla ya urefu wa kilomita 300, inajengwa na Kampuni ya Kituruki ya Yapi Merkezi kwa ubia na Kampuni ya Mota-Engil Africa ya Ureno.

Mgedzi alisema kuwa, ujenzi wa reli hiyo ulianza kwa kufanya usanifu wa njia ya reli itakapopita kwa maana ya kutafiti udongo, madaraja, kiwango cha maji yatakayokuwa yakikatisha kwenye madaraja na makalveti.

Mbali na utafiti huo, shughuli nyingine ambayo walikuwa wakiendelea nayo ni kupata ardhi kwa maana ya kuthamini ardhi na mali za watu ambapo reli itapita, na kinachofanyika kwa sasa ni ujenzi wa miundombinu na reli yenyewe. Usimamizi wa ujenzi Ili kuhakikisha ujenzi wa reli hiyo unakidhi viwango na ubora uliokusudiwa, Meneja wa Mradi huo alisema kuwa mkandarasi ambaye ni Kampuni ya Kituruki ya Yapi Merkezi unasimamiwa na mhandisi mshauri au mshauri elekezi ambaye ni Kampuni ya Kikorea ijulikanayo kama Korail JV kwa niaba ya Rahco.

Kampuni hiyo, imeelezwa kuwa na wataalamu wapatao 47 wenye uwezo wa kusimamia ujenzi wa miundombinu pamoja na mifumo mbalimbali. Uwezo wa Mkandarasi Kuhusu uwezo wa mkandarasi katika kutekeleza na kukamilisha mradi huo kwa wakati, imeelezwa kuwa mkandarasi ameweza kuleta nchini mitambo 241 ambayo inafanya kazi eneo la ujenzi lakini pia ana mitambo mingine midogo midogo 218 ambayo nayo inaendelea na kazi na hivyo kufanya idadi yote ya mitambo inayotumika kwenye ujenzi huo kufikia 459.

Kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa na Rahco wakati wa zabuni na kwa uhakiki walioufanya kwa kutembelea miradi ambayo Mkandarasi ameshaifanya kwenye baadhi ya nchi, Mgedzi alisema kuwa wamejiridhisha uwezo wa Mkandarasi hauna mashaka. Alisema, mbali na miradi ambayo ameshaitekeleza kwenye baadhi ya nchi, lakini kampuni hiyo pia inashika nafasi ya 78 kati ya makandarasi bora wa ujenzi duniani kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2017.

“Mkandarasi huyu ameshafanya kazi za miradi ya reli na miradi ya reli ya mwendokasi 51 katika nchi nyingi duniani ikiwemo Ethiopia, Qatar, Morocco, Saudi Arabia, Falme za Kiarabu, Msumbiji, Uturuki na Marekani,” alieleza Mgedzi.

Ujenzi wa uzio Kwa lengo la kuhakikisha watu wanakuwa salama na treni zinafanya safari zake kwa usalama muda wote, Rahco imekusudia kujenga uzio kuanzia mwanzo hadi mwisho wa reli hiyo.

Uzio huo umeelezwa kuwa utasaidia kuzuia ajali kutokana na watu na wanyama kukatisha reli. Mgedzi alisema, kwa kuwa treni ya abiria itakuwa ikikimbia kwa mwendokasi wa kilomita 160 kwa saa na ile ya mizigo kilomita 120 kwa saa, hivyo mtu au mnyama atakayekatiza hapo hatabaki hai, lakini pia wanaweza kusababisha ajali kwa treni na maafa makubwa kutokea kwa sababu treni hiyo haina uwezo wa kusimama kwa ghafla.

Mbali na kusababisha ajali, Mgedzi pia alisema kwa kuwa reli hiyo itahusu matumizi ya mifumo ya umeme, inaweza kuwa hatari pia kwa watu kama uzio hautajengwa. Ajira kwa wazawa na wageni Suala la ajira kwa Watanzania ni muhimu hasa linapokuja suala la miradi mikubwa kama huo wa ujenzi wa reli ya kisasa.

Aidha, Mgedzi alisema kuwa mkandarasi anatoa fursa ya kazi ndogondogo kama vile kazi za ujenzi na ugavi kwa maana ya kupeleka vifaa vya ujenzi na mitambo, hivyo Watanzania wenye kampuni kama hizo wanapaswa kujitokeza ili waweze kufanya kazi na Mkandarasi. Ununuzi wa vichwa na mabehewa Kwa mujibu wa meneja wa mradi huo, zabuni kwa ajili ya ununuzi wa mitambo, mabehewa na vichwa vya treni vitakavyotumika kusafirisha abiria na mizigo kwenye reli hiyo ya kisasa ilishatangazwa mwishoni mwa Mwezi Desemba mwaka jana.

Menaja huyo alisema kuwa manunuzi mengine kama vile ya reli inayojengwa, kokoto, saruji na vifaa vingine vyote vya ujenzi, na vifaa vya miundombinu ya umeme na mawasiliano vinannunuliwa na Mkanadarasi mwenyewe kwa kuzingatia matakwa ya mkataba. Wataalam wa Kitanzania Ili kuhakikisha mradi huo wa reli ya kisasa unaendeshwa na watu wenye uwezo na sifa inayotakiwa, Mgedzi alisema kuwa mipango iliyopo sasa ni kuwaandaa wataalam wazawa watakaoweza kuendesha na kusimamia mradi huo.

Alisema wana mipango ya kuajiri na kuwasomesha wataalam hao nje na ndani ya nchi ili wapate ujuzi mwafaka wa kuendesha na kusimamia treni hiyo. Gharama za mradi Mradi huo wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro umeelezwa kujengwa kwa gharama ya Sh trilioni 2.7 ambazo zote ni fedha za Serikali.