Bomoa bomoa ya ujenzi holela Dodoma yaanza

MANISPAA ya Dodoma, jana ilianza shughuli ya kubomoa nyumba za makazi, biashara na huduma mbalimbali ambazo zimejengwa bila kuwa na kibali.

Pamoja na kukosa kibali nyumba nyingi zilizoanza kubomolewa jana ni zile ambazo zimekiuka utaratibu wa mipango miji. Kazi hiyo ya ubomoaji inafanyika baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk Binilith Mahenge, kutembelea maeneo ya Kikuyu Kusini mwishoni mwa wiki kuona ujenzi holela na kuagiza utaratibu ufanyike wa kubomoa 20% 60% nyumba hizo.

Aidha, aliagiza nyumba hizo zianze kubomolewa kuanzia jana Jumanne, kazi ambayo imeanza kutekelezwa na Manispaa. Aliagiza Manispaa kukomesha ujenzi holela Dodoma na kwamba shughuli hiyo ya ubomoaji imelenga kuhakikisha kwamba wananchi na wataalamu wanaheshimu mipango miji. Katika shauri la ubomoaji, Mkuu wa Mkoa Dk Mahenge alitaka kikosi kazi alichotaka kiundwe kukabiliana na ujenzi holela kufanya kazi hiyo na kuacha kuigeuza Dodoma kama Manzese.

Miongoni mwa maeneo ambapo bomoabomoa hiyo imefanyika ni Uwanja wa Ndege, eneo la baa ya Chako ni Chako, nyumba za makazi eneo la Kikuyu Kusini, Kikuyu Extension na Majengo Kisasa. Pamoja na vibanda vilivyojengwa karibu na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma. Oparesheni hiyo pia iligusa nyumba za biashara zaidi ya 20 zilizojengwa kwenye hifadhi ya barabara ya Dodoma- Dar es salaam eneo la Kisasa.

Mwandishi wa gazeti hili, alishuhudia ubomoaji huo huku wananchi wakionekana kuhaha kuokoa mali zao ili zisiharibiwe na tingatinga lililokuwa likifanya kazi ya ubomoaji. Akizungumzia shughuli hiyo, Ofisa Udhibiti Uendelezaji Ujenzi wa Majengo Manispaa ya Dodoma, Ally Bellah alisema ubomoaji wa awamu ya kwanza utadumu kwa siku mbili.

Alisema, maeneo yote ambayo ubomoaji unafanyika walishatoa Ilani za kubomoa lakini wahusika walikataa kutii amri na kuendeleza maeneo kinyume na utaratibu. Bellah alitaka kazi ya ubomoaji kufanyika kwa nidhamu na endelevu na maeneo yaliyotengwa kwa shughuli husika zinatakiwa kubaki kwa shughuli hizo na atakayefanya kinyume atachukuliwa hatua.

Aliwataka wananchi kuhakikisha kwamba wanafanya ujenzi wenye kufuata utaratibu pamoja na kupata vibali. Alisema, wakati ufike mji upewe hadhi yake ya Makao Makuu kwa kuwa na mji uliopangika na hilo litawezekana kama wananchi wataacha ujenzi holela. Katika eneo Magharibi moja ya nyumba ilibomolewa huku wapangaji wakiwa hawana taarifa na ubomoaji huo.Walisema kitendo walichofanyiwa na mwenye nyumba hiyo si cha kiungwana kwani alikuwa na taarifa lakini alishindwa kusema ukweli.